METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 20, 2021

WANANCHI WA SUGUTI, KATARYO WAIPONGEZA TARURA KWA UJENZI WA DARAJA

Muonekanao wa daraja la awali lililokuwa linatumiwa na wakazi wa Kata ya Suguti na Kataryo lililopo katika barabara ya Wenyere – Kataryo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara.

Muonekanao wa daraja jipya la chuma lililoanza kutumiwa na wakazi wa Kata ya Suguti na Kataryo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, mkoani Mara. Daraja hili lipo Mto Suguti barabara ya Wenyere – Kataryo.

Na. Erick Mwanakulya, TARURA.

Wananchi wa Kata ya Suguti na Kataryo zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya Musoma, mkoani Mara wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), baada ya kutatuliwa kero yao ya muda mrefu kwa kujengewa Daraja la chuma katika Mto Suguti uliopo barabara ya Wanyere Kataryo.

Wakizunguma katika mahojiano maalum, wananchi wa Kata ya Suguti walisema kuwa hapo awali kulikuwa na daraja la miti ambalo lilikuwa linahatarisha usalama wao hasa kipindi cha masika na kukatisha mawasiliano hivyo kushindwa kufika Wanyere ili kuweza kupata mahitaji yao na huduma za kijamii kama shule, hosptali na masoko.

“Tunaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa Daraja ili la Suguti sasa kwenda Kataryo si kikwazo tena watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule hasa katika kipindi cha masika, tulikuwa hatuwezi kwenda upande wa pili na kusubiri maji yapungue hata siku tatu mpaka nne ndipo tuweze kwenda Wenyere kupata huduma za kijamii, kwa kweli tunaishukuru sana Serikali”, alisema Ndg. John Changulu mkazi wa Wanyere.

Bw. Moshi Maligesi ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Wanyere ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Samia S. Hassan kwa jitihada zake anazoendelea kuzifanya katika kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini ili kuimarisha utendaji kazi wake wa kuboresha miundombinu katika maeneo mbalimbali.

“Eneo hili la Mto Suguti ilikuwa ni shida sana kuvuka kwenda upande wa pili hasa katika kipindi cha masika watoto walishindwa kwenda shule na wajawazito walishindwa pia kufika hospitalini kupata huduma, kwani mawasiliano huwa yanakatika kabisa, ila kwa ujenzi huu wa daraja tunaishukuru sana TARURA.

Naye, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Mhandisi Hussein Abbas alisema kuwa ujenzi wa daraja la chuma la Saguti katika Mto Saguti umegharimu shilingi milioni 80 lenye urefu wa Mita 24 ambapo ujenzi wa daraja hilo umepewa kipaumbele kwani ni muhimu kwa wananchi wa Suguti na Kataryo katika kupata mahitaji yao ya kila siku kwa kuwa wananchi hao wanategemea kupata huduma katika Kijiji cha Wanyere.

Kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo la Suguti ni sehemu ya mikakati ya TARURA ya kuboresha huduma ya usafiri na usafirirshaji hasa kwa maeneo ya pembezoni ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Wakala umejipanga kuhakikisha unawafungulia huduma wananchi ili mahali maliposhindwa kufikika sasa pafikike  na hii ni baada ya Serikali kuongeza bajeti ya Wakala.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com