Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akipokea zawadi ya Batiki kutoka kwa Wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha wanaojishughulisha na mafunzo kwa vitendo alipofika Chuoni hapo akiwa ziarani Mkoani Iringa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, anayeshughulikia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Neema Ndoboka akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kuhusu Kituo cha kidigitali cha Ubunifu na Maarifa kilichoanzishwa katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Estomih Kyando.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa katika ziara yake katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo mkoani Iringa.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
…………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu, Iringa
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini vimetakiwa kuandaa mazingira rafiki na wezeshi kwa wahitimu wake ili waweze kuajirika, kujiajiri na kuwaajiri wengine mara baada ya kuhitimu masomo yao.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika ziara yake katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Mkoani Iringa.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema kuwa lengo la uwepo wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini ni kusaidia wanafunzi kupata ujuzi na utaalamu wa masuala ya maendeleo ya jamii yatakayowasaidia katika kupata ajira na kujiajiri wenyewe
“Nimetembelea maonesho mbalimbali chuoni hapa na kushuhudia kazi za mikono ya wanavyuo na zinatia moyo. Nakuagiza Mkuu wa Chuo kwa kushirikiana na viongozi wengine, watafutie masoko na kuwaunganisha na taasisi nyingine ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na hivyo kuondokana na umasikini” alisema Naibu Waziri Mwanaidi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini ili kuhakikisha vinasaidia kutoa wataalam wa Maendeleo ya Jamii wakataosadia kuleta mabadiliko na kutatua changamoto za jamii inayowazunguka
Wakizungumza kwa nyakati tofauti chuoni hapo baadhi ya wanachuo na wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo wameeleza kuridhishwa na jitihada za Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha katika kubuni na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za ujasiriamali zinazowawezesha kujikwamu kiuchumi na kuendeleza familia na jamii zao.
Hata hivyo wamesema pamoja na hatua ya mafanikio ilivyofikiwa, bado wanakabiliwa na changamoto ya mtaji na zana za kisasa katika kuendesha shughuli za ubunifu hivyo wamaeiomba Serikali ione namna bora ya kuwezesha wajasirimali kupata unafuu katika zana za kisasa.
Akiwasilisha taarifa ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha, Mkuu wa Chuo hicho Godfrey Mafungu amesema pamoja na changamoto kadhaa zinazojitokeza, Chuo kinatumia wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutoa mafunzo na kusambaza elimu ya ujasiriamali kwa wanachuo na jamii ili kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kujileta maendeleo.
Akiwa Chuoni hapo, Naibu Waziri Mwanaidi alikagua shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukarabati wa Jengo la Utawala, Ukumbi wa mihadhara pamoja na Jengo maalum la Kituo cha Kidigitali cha Ubunifu na maarifa.
0 comments:
Post a Comment