Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande (Kushoto) akipata maelezo kuhusu za uchimbaji wa makaa ya mawe na hifadhi ya mazingira kutoka kwa Bw. Edward Mwanga Meneja wa Mgodi wa TanCoal ulipo Mbinga. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Bi. Aziza Mangosongo
Bw. Ryan Wienard Mkurugenzi wa Ruvuma Coal Ltd akitoa maelezo ya shughuli za uchimbaji makaa ya mawe mgoni hapo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande na ujumbe wake. Naibu Waziri Chande yuko Mkoani Ruvuma kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Picha ikionyesha eneo linalochimbwa Makaa ya mawe katika mgodi wa Ruvuma Coal
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande (Kulia) akifurahia jambo na Bi. Esha Kapinga Mkazi wa Namtumbo mara baada ya Naibu Waziri Chande kufanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji vya Mto Luegu na juhudi za kuhifadhi vyanzo hivyo katika ukaguzi uliofanyika leo 13/07/2021.
Na Lulu Mussa,Ruvuma
Serikali imesema uwekezaji wowote ni lazima uzingatie Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake ikiwa ni pamoja kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa kuwa ni takwa la Kisheria.
Hayo yamesemwa leo Wilayani Mbinga na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande mara baada ya kufanya ziara ya kukagua migodi ya uchimbaji wa Makaa ya mawe ya Tancoal Ltd na Ruvuma coal.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Chande ametoa siku 14 kwa Mgodi wa Tancoal kudhibiti maji taka katika mabwawa yao pamoja na kudhibiti vumbi ambalo limekuwa kero kwa wakazi wa maeneo ya jirani.
“Mazingira ndio uhai wetu, tuyatunze na tuyalinde kwa gharama yoyote ile” Chande alisisitiza.
Chande ameshuhudia ukataji wa miti kwa kiwango kikubwa katika migodi hiyo na kuwaagiza migodi yote miwili kuandaa mpango wa muda mfupi wa upandaji miti ili kurejesha uoto wa asili.
Aidha, Naibu Waziri Chande ameagiza migodi hiyo ya makaa ya mawe kuhakikisha wanaanda na kutekeleza mpango madhubuti wa kurejesha ardhi katika hali ya awali mara baada ya shughuli za uchimbaji kukamiika ikiwa ni pamoja na kupanda miti kwa wingi.
“Upandaji miti uwe ni utamaduni wetu, hapa mgodini miti mingi imekatwa, wekeni mkakati wa kuirejesha kipindi cha mvua” Chande aliagiza.
Katika hatua nyingine Waziri Chande amemuagiza Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Kusini Bw. Jamal Baruti kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha masuala ya Uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira yanakuwa endelevu.
Akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Mbinga Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Aziza Mangosongo amesema jitihada na mikakati mbalimbali imechukuliwa katika kudhibiti vitendo vya uchafuzi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za uchimbaji wa madini kwa kufanya ufutiliaji na usimamizi wa mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
Uchimbaji, uchakataji na uuzaji wa madini ya makaa ya mawe Wilayani Mbinga zilianza mwaka 2012 kupitia Kampuni ya TanCoal Energy Ltd na siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la Kampuni nyingi zinazojikita katika utafiti na uwekezaji kwenye sekta ya madini.
0 comments:
Post a Comment