Picha ya pamoja baina ya wawezeshaji, viongozi wa Serikali na washiriki wa mafunzo ya namna bora ya uchukuaji sampuli kwa ajili ya uchunguzi na uchenjuaji wa madini yanayotolewa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Mkoani Mtwara.
Mchimbaji wa madini Ahamed Waziri kutoka Machimbo ya Lupaso Wilaya ya Masasi-Mtwara akiuliza maswali kwa wawezeshaji wa mafunzo ya namna bora ya uchukuaji sampuli kwa ajili ya uchunguzi na uchenjuaji wa madini yanayotolewa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Mkoani Mtwara
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Moses Machali akiangalia kitabu cha mwongozo wa namna bora ya uchukuaji wa sampuli kwa ajili ya uchunguzi na uchenjuaji wa madini kilicho andaliwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mara baada ya kufungua mafunzo hayo Wilayani Masasi, Mkoani Mtwara
Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Mtwara- MTWAREMA Abdallah Esmail akiuliza maswali katika mafunzo ya uchukuaji wa sampuli za madini na miamba yaliyotolewa bure na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) katika wilayaya Masasi Mkoani Mtwara.
Mhandisi Uchenjuaji Lilian Anton kutoka GST akitoa mafunzo ya namna bora ya uchukuaji sampuli kwa ajili ya uchenjuaji wa madini kwa wachimbaji wadogo Mkoani Mtwara, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Na Projestus Binamungu, Idara ya Habari Maelezo
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inaendesha mafunzo ya siku tatu kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mtwara juu ya namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa madini, kama sehemu ya kuwawezesha wachimbaji hao kufanya shughuli zao kisasa na kisayansi zaidi, ili kuongeza tija na mapato katika kazi yao.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Moses Machali aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuungana ili waweze kumudu gharama mbalimbali zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji madini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa, kupata mikopo na kumudu vipimo mbambali vya madini kabla hawajaanza kuchimba.
Alisema “Tutoke kwenye uchimbaji wa madini kama mtu na sasa tuwe kampuni, au kikundi kikubwa kinachoweza kuaminika mbele ya taasisi za fedha na hata kukopesheka kiurahisi.”
“Kuna baadhi ya wachimbaji wamechimba madini miaka 10 mpaka 20, wengine mpaka kifo bila kuyafikia mafanikio au ndoto zao, hii kwa sehemu kubwa inatokana na kufanya uchimbaji kwa imani tu bila vipimo, jamani madini siyo uchawi wala majini, lazima tukubali kuitumia taaisi yetu ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili itupemie ardhi na kutufanyia tathimini ya thamani ya kilichopo chini ya ardhi tunayotaka kuichimba kabla hatujawekeza nguvu na pesa yetu” alisema Machali.
Awali akiongea kwa niaba ya wachimbaji wadogo Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Mtwara- MTWAREMA Abdallah Esmail alisema, mafunzo hayo wanayahitaji karibia wachimbaji wote wa madini nchi nzima na kiomba GST iweke utaratibu angalau wa kutoa mafunzo hayo kila baada ya miezi mitatu ili kuwajengea uwezo zaidi wachimbaji na kuwakumbusha juu ya taratibu zinazo hitajika kufuatwa kitaalam katika uchukuaji wa sampuli.
“Tunaishukuru Serikali kwa kugharamia mafunzo ya uchukuaji wa sampuli za madini na miamba bure kwa wachimbaji wadogo hapa kwetu Mtwara, mara ya mwisho mafunzo ya aina hiyo yaliendeshwa mkoani Lindi kwenye kanda yetu ya kusini na washiriki tuligharamia shilingi laki tano, Kwakweli ahsanteni GST. Alisema Esmail
Katika mafunzo hayo yaliyowakutanisha wachimbaji wa madini zaidi ya 100 mjini Masasi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara Mjiolojia Zortosy Mpangile ambaye ni mmoja wa wawezeshaji katika mafunzo hayo alisema GST imegundua wachimbaji wengi wa madini wanachukua sampuli kiholela pasipo kuzingatia taratibu za uchukuaji wa sampuli inayokwenda maabara, na kwakufanya hivyo tayari wanakuwa wameathiri majibu ya vipimo vya sampuli zao.
Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa yenye aina mbalimbali za madini na wataalam kutokaGST wameyainisha maeneo yenye madini katika mkoa huo kuwa ni pamoja na Lupaso, Chipite, Nanyumbu, Naugoo, Chikundi, na Mbaju.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment