VIONGOZI wa umoja wa vijana wa mkoa wa Iringa wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa, Majungu, makundi na fitina katika kuongoza jumuiya hiyo ambayo ndio tanuli la kuwapika viongozi bora wa chama cha mapinduzi na serikali kwa ujumla kwa ajili ya kuja kuliongoza taifa.
Akiongea kwenye mkutano mkuu maalum wa uchaguzi wa kujaza nafasi ya mwenyekiti wa umoja wa vijana wa mkoa wa Iringa, mwenyekiti mstaafu wa UVCCM mkoani humo ambaye ni mkuu wa wilaya ya Arusha Kenani Kihongosi alisema kuwa ili kuwa na jumuiya ya vijana bora ambayo itapika vilivyo viongozi bora ni lazima kuhakikisha wanaendeleza ushirikiano ulikuwepo kwa viongozi wa chama na serikali.
Alisema kuwa kiogonzi wa umoja wa vijana akiendekeza Majungu, makundi na mpenda rushwa hawezi kuwa kiongozi bora kwenye kuimalisha umoja wa vijana ambao ndio tanuli la kuwapika viongozi bora.
Kihongosi aliongeza kwa kuwashauri viongozi wa umoja wa vijana mkoa wa Iringa kuendelea kuilinda ilani ya chama cha mapinduzi na katiba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kudumusha umoja na amani ambao umedumu kwa miaka mingi.
Aliwaomba viongozi waliochaguliwa kuingoza jumuiya ya umoja wa vijana mkoa wa Iringa Uchaguzi usiwagawe bali ukawaunganisha upya kuwa na umoja utakaodumu kwa kipindi chote watakacho kuwa madarakani.
Kwa upande Meya wa manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada amewataka vijana kuwa na ushirikiano kuanzisha vikundi vitakavyo wawezesha kupata mikopo ya asilimia 4 ya vijana badala ya kuendelea kuwa na makundi ya majungu.
Ngwada alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakilalamika masuala ya ajira badala yakuanzisha vikundi vya ujasiriamali ambayo vitawawezesha kupata mikopo ya halmashauri ambayo hutolewa na serikali bila riba.
“mikopo ile ya vijana inayotolewa na halmashauri ni yetu sisi vijana tuchangamkie fursa wakina mama wamekuwa kila siku wakija pale halmashauri kuomba mkopo lakini ukiangalia vijana wao wapo tu kulalamika hatuna mitaji anzeni sasa na serikali itawashika mkono” alisema Ngwada.
Akizungumza kamisaa wa CCM mkoa wa Iringa ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kujiongezea ufahamu badala ya kufanya mijadala ambayo huleta uchonganishi kwa taifa na jamii.
Alisema kijana mwenye maono huondoa uoga na katika kutafuta maendeleo na hutumia mitandao ya kijamii ili kujijengea uelewa wa kuchanganua masala mabalimbali ya maisha pamoja na jamii inayomzunguka .
Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa kujaza nafasi ya mwenyekiti,msimamizi wa uchaguzi huo mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa MNEC wa njombe Fidelis Lumato alimtangaza Anord Mvamba kuwa ndio mwenyekiti mpya baada ya kupata jumla ya kura 181 za kutoka kwa wajumbe wote wa umoja huo.
Alisema kuwa jumla ya kura 329 zilipigwa na hakuna kura halali zilizoharibika hivyo mshindi wa kwanza Anord Mvamba alipata 181 na mshindi wa pili Fatma Rembo alipata 123 huku wa tatu Iazack Mgovano alipata kura 25
Alimalizia kwa kuwaomba vijana wote wa umoja huo kuvunja makundi yote waliyokuwa nayo na kuanza kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuendelea kuijenga jjumuiya hiyo kuwa imara kama ilivyokuwa awali.
Baada ya ushindi huo mwenyekiti mpya wa UVCCM mkoa wa Iringa Anord Mvamba alisema kuwa ataendeleza maono ya mwenyekiti mstaafu ya kuhakikisha vijana wanakuwa na umoja na mshikamano.
Aliwataka vijana kuvunja makundi yote yaliyotokana na uchaguzi ili kuhakikisha wanakijenga chama na kutafuta fursa mbalimbali zitakazowainua kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment