METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 2, 2019

MABARAZA YA ARDHI YA KATA NA VIJIJI YASIYOTENDA HAKI MAFIA YAVUNJWE-DKT MABULA


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Baleni wilayani Mafia mkoa wa Pwani alipokwenda kusikiliza kero za ardhi katika eneo hilo akiwa katika ziara yake ya siku mbili katika wilaya hiyo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua masijala ya ardhi jana.
Mwananchi Hassan Omar maarufu mzee wa Lumbesa mkazi wa Dagoni Mafia akimuonesha nyaraka Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kuhusiana na mgogoro wa ardhi wakati Dkt Mabula alipofanya ziara wilaya ya Mafia  kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua masijala ya ardhi jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua Majalada ya Ardhi katika ofisi ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mafia jana wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua masijala ya ardhi jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mafia Shaib Nnenduma na Kulia ni Afisa Ardhi Chuchu Ochere.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia baadhi ya Nyaraka za umiliki wa ardhi kutoka kwa Hassan Mohamed (Kushoto) na Mwanangano Mohamed wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi katika wilaya ya Mafia jana (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
…………………………
Na Munir Shemweta, WANMM MAFIA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Erick Mapunda kuyavunja Mabaraza yote ya Kata na Vijiji ya ardhi yasiyotenda haki wakati wa kutoa maamuzi katika wilaya ya Mafia mkoani Pwani.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo jana akiwa katika ziara yake ya siku mbili wilayani Mafia mkoani Pwani kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua masijala ya ardhi.
Alisema, kutokana na kero nyingi za ardhi alizozipokea katika ziara yake hiyo wilayani Mafia amebaini Mabaraza ya Kata na Vijiji katika wilaya hiyo hayafanyi kazi zake vizuri na wajumbe wake wamekuwa wakiyatumia kutoa maamuzi yasiyotenda haki.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, kadri Mabaraza ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia yanavyofanya vibaya katika utoaji maamuzi yake basi hata uanzishwaji Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya hiyo halitafanya vizuri katika utendaji wake.
‘’Ukiwa na watu wasioweza kusimamamia haki itakuwa shida sana, Mkurugenzi hakikisha Mabaraza ya Ardhi katika Kata na Vijiji yasiyofuata taratibu na kutoa haki kwa walalamikaji unayavunja na kuteua wajumbe wapya’’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi alitaka kupitiwa upya Mabaraza yote ya ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia hasa yale yanayolalamikiwa na kubainisha kuwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko tayari kutoa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba nchini ili atoe elimu katika Mabaraza hayo kwa lengo la kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Alisema, Mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia hayatendi haki na wakati mwingine Baraza la Kata linachukua kesi ya Baraza la Kijiji lengo likiwa kutotenda haki kwa walalamikaji.
Baadhi ya wananchi wa Mafia wamelalamikia Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi kuwa wajumbe wake hawatendi haki wakati wa kutoa maamuzi na hivyo kuonesha dhahiri uwepo dalili za rushwa.
Mohamed Shaban alimueleza Dkt Mabula kuwa, Mabaraza ya ardhi ya Kata wakati mwingine hayatendi haki na kumtaka anayeshindwa kesi kwenda Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya la Mkuranga huku wakijua mlalamikaji atashindwa kwenda Mkuranga kutokana na changamoto za usafiri na hivyo kupoteza haki yake.
Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Erick Mapunda alieleza kuwa Mabaraza ya ardhi ya Kata na Kijiji katika wilaya hiyo yapo na yanafanya kazi na wajumbe wake wamewezeshwa kwa kupatiwa mafunzo ingawa alieleza changamoto iliyopo Baraza katika kata ya Kilindoni ambalo alilileleza kuwa badala ya kuatatua matatizo limekuwa chanzo cha migogoro kwa kuwa wakati mwingine hufanya mashauri yaliyo nje ya kata yake na suala hilo tayari alishalitolea agizo la kuvunjwa kwa baraza
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com