METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 5, 2021

MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA YATOA MIFUKO 200 YA SARUJI JIMBO LA NSIMBO

Na Mathias Canal, Katavi

Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania imetoa mifuko 200 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa ajili ya kusaidia kuboresha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika jimbo la Nsimbo mkoani Katavi.

Akikabidhi mifuko hiyo Meneja wa Uwanja wa Ndege Mpanda Bw. Jeff  Shantiwa amesema kuwa wametoa mifuko hiyo kama sehemu ya kusaidia jamii wanayoihudumia na kuunga juhudi zinazofanyika kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa saruji hiyo Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Anna Lupembe amemshukuru Mkurugenzi wa Viwanja Vya ndege Tanzania kwa kuona umuhimu wa kusaidia jamii na kuzitaka taasisi nyingine kushiriki katika kuleta maendeleo katika jamii.

Lupembe amesema kuwa mifuko hiyo itasaidia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa na Hosteli zinazoendelea kujengwa katika jimbo hilo huku akikabidhi viongozi wa Kata ya Machimboni mifuko 50 kwa ajili ya shule ya msingi Kapanda na Shule ya Sekondari Machimboni.

Akitoa shukrani Mwenyekiti wa Kijiji cha Kapanda Bw. Robert Katani amesema kuwa msaada huo utasaidia katika kukamilisha ujenzi wa Shule ya Msingi Kapanda kijiji ambacho hakina shule ya msingi na kusababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kufika shuleni.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com