Kiongozi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Inyonga Padri Maricelo Butoyi akiongoza Misa Maalumu ya kumuombea Hayati Dkt John Pombe Magufuli, tarehe 24 Machi 2021.
Na Mathias Canal, Mlele-Katavi
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe Jamila Yusuph amesema Wilaya ya Mlele itamkumbuka aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli kwa Maendeleo aliyoyafanya.
Mhe Jamila ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye Misa maalumu ya kumuombea Dkt Magufuli iliyofanyika leo tarehe 24 Machi 2021 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Inyonga Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi.
Dc Jamila amesema kuwa miongoni mwa mambo mahususi ambayo wananchi watamkumbuka kwa kina Hayati Dkt Magufuli ni pamoja na Uimarishwaji wa huduma za Afya, Miundombinu ya Barabara, Mawasiliano na Uchukuzi, Uboreshwaji wa Huduma za Maji, Sekta ya Elimu ikiwa ni pamoja na Miradi ya Umeme mijini na vijijini.
Kadhalika DC Jamila ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupokea kijiti katika kipindi cha majonzi huku akiamini kuwavusha watanzania kufikia katika dhamira ya Tanzania waitakayo.
Akizungumza wakati wa Ibada hiyo Kiongozi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Inyonga Padri Maricelo Butoyi amesema ili kumuenzi Hayati Dkt John Pombe Magufuli ni lazima kuyaenzi matendo yake kwa kuwa wazalendo hususani kukemea vitendo viovu ikiwemo Rushwa na ubadhilifu wa mali za umma.
Padri Butoyi, amewaomba wananchi kutumia muda wao kufanya ibada ya kuwaombea Viongozi wa Serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe Rachel Kasanda anayeendelea na matibabu pamoja na Taifa kwa ujumla wake.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhe Soud Mbogo amewaomba wananchi kumtanguliza Mungu na kufanya matendo mema aliyokuwa akiyafanya Hayati Rais Magufuli.
Kadhalika, amelipongeza Kanisa Katoliki Parokia ya Inyonga kwa kuendesha misa maalumu ya kumuombea Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment