Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Serikali kwa kuwawezesha vijana kupata ujuzi kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo imekuwa chachu kwa vijana kujiajiri na kuajiri wenzao.
Hayo yameelezwa na wajumbe wa kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipokutana na kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi Bungeni Dodoma, Machi 11, 2021.
Akizungumza Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) alieleza kuwa Programu hiyo ya Kukuza Ujuzi inayotekelezwa na Serikali imeweza kuwezesha vijana wengi kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi kutokana na mafunzo ya stadi za kazi wanayopatiwa vijana hao.
“Pragramu hii muhimu sana katika kuiwezesha nguvu kazi ya taifa hasa vijana kuwa na ujuzi stahiki na hivyo wataweza kujiajiri na kuajiri wenzao, tunaipongeza serikali kwa mkakati huu na pia tunawasihi muongeze wigo wa kuwafikia vijana zaidi,” alisema Mchengerwa
Awali akitoa maelezo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alieleza kuwa Programu hiyo ya kukuza ujuzi nchini imetokana namakubaliano kati ya Serikali na Sekta binanfsi kupitia mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ambapo waajiri wengi walisisitiza kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuhakikisha nguvukazi ya taifa inakuwa na ujuzi stahiki.
“Utekelezaji wa programu hii ni hatua za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvukazi inayohitajika kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi ili kumudu ushindani wa soko la ajira la ndani na nje ya nchi,” alisema Katambi
Aliongeza kuwa, kutokana na utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 ulionesha takriban asilimia 79.9 ya nguvukazi ya taifa ina kiwango cha chini cha ujuzi, asilimia 16.6 ya nguvukazi ina kiwango cha kati cha ujuzi na asilimia 3.6 ya nguvu kazi ina kiwango cha juu.
Alisema, Matokeo ya tafiti hizo ilithibitisha kuwa kuna umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana kushiriki kwao katika mipango ya maendeleo ikiwemo uanzishaji na utekelezaji wa programu maalum za kukuza ujuzi na maarifa kwa kundi hilo.
“Mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha ifikapo 2025/2026 nguvu kazi ya taifa inakuwa na kiwango cha ujuzi stahiki ili kumudu ushindani wa soko la ajira pamoja na kuhakikisha sekta mbalimbali katika uchumi wa taifa zinakuwa na wataalam wa kutosha,” alieleza
Naye Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ally Msaki ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi alisema kuwa Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kutekeleza Programu ya miaka mitano ya kukuza ujuzi nchini (2015/2016 – 2019/2020) iliyokusudia kuwezesha nguvukazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili waweze kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.
Msaki aliongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2019/2020 jumla ya vijana 65,008 wamenufaika kupitia programu hiyo ya kukuza ujuzi kupitia mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo usio rasmi, mafunzo ya vitendo mahala pa kazi katika fani mbalimbali walizosomea, pamoja na mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba.
0 comments:
Post a Comment