METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, March 6, 2021

DKT. KALEMANI AZINDUA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA MAGARI YA DANGOTE

Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (katikati) akimueleza jambo Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) alipofanya ziara ya kukagua mitambo ya kupoza umeme katika Kituo cha Mtwara, alipofanya ziara Mkoani humo, Machi 5, 2021.

Vifaa maalum vya kudhibiti hitilafu ya umeme vikiwa vimefungwa katika nguzo za kusafirisha umeme, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliagiza vifaa hivyo vifungwe katika maeneo yote nchini, alipofanya ziara Mkoani Mtwara, Machi 5, 2021. 

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akiangalia  kiwango cha gesi asilia kinachoingia kinachojazwa katika moja ya magari ya kampuni ya kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote, baada ya kuzindua matumizi ya gesi asilia katika magari ya kampuni hiyo, alipofanya ziara mkoani Mtwara Machi 5, 2021.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akionyeshwa namna gesi asilia inavyojazwa katika matanki ya magari yanayotumia gesi asilia ya kampuni ya kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote baada ya kuzindua matumizi ya gesi asilia katika magari ya kampuni hiyo, alipofanya ziara mkoani Mtwara Machi 5, 2021.

Na Zuena Msuya Mtwara

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua matumizi ya Gesi asilia katika magari (CNG) ya kampuni ya kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote katika kufanya safari zake badala ya kutumia mafuta.

Dkt. Kalemani alifanya uzinduzi huo wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Mtwara ya kutembelea Kiwanda cha Dangote, kukagua Kituo cha Kupoza Umeme cha Mtwara na kutembelea Kisima cha Gesi Asilia cha Ntorya iliyofanyika Machi 5, 2021.

Alisema kuwa kiwanda hicho kimepanga kuunganisha jumla ya magari 600 kutumia gesi asilia, ambapo katika awamu ya kwanza tayari wameunganisha magari 250, awamu ya pili wataunganisha magari 350.

Hata hivyo Dkt. Kalemani aliushauri uongozi wa kiwanda hicho kuunganisha magari yake yote takribani 1000 kutumia gesi asilia katika safari zake badala ya mafuta.

Mradi wa kusindika gesi asilia katika kiwanda cha Dangote umegharimu fedha za kitanzania shilingi Bilioni 21, kuanzia hatua za awali hadi kukamilika kwake.

“Matumizi ya gesi ni nafuu yanapunguza takribani 45% ya gharama kiuendeshaji ukilinganisha na mafuta, pia hailipuki na ni rafiki kwa mazingira, nawasihi wenye magari wote, Pikipiki, Bajaji na vyombo vyote vya moto kutumia gesi asilia katika uendeshaji wake”, alisema Dkt. Kalemani.

Vilevile alisema kuwa matumizi ya gesi asilia nchini, bado hayajafikia asilimia moja ya gesi yote inayogundulika nchini licha ya asilimia 60% ya umeme unaotumika nchini kutokana na gesi hiyo yenye futi za ujazo zaidi ya Trilioni 57 mpaka sasa.

Dkt.Kalemani alisema kuwa, mpango wa Serikali ni kusambaza gesi asilia nchi nzima na kueleza kuwa Mikoa ambayo kijiografia haitakuwa rahisi kufikiwa yatajengwa matanki makubwa katika vituo maalumu ili kuhifadhi na kusambaza gesi hiyo sehemu mbalimbali.

Serikali imeanza kutoa fursa kwa wawekezaji binafsi, kuwekeza katika biashara ya CNG, zikiwepo kampuni zenye vituo vya kuuza mafuta ambazo zitaweza kufunga pampu za kujaza gesi kwenye magari katika vituo hivyo.

Zaidi ya Kampuni sita (6) tayari zimepewa idhini ya kuendelea na biashara hiyo na zipo katika hatua ya kuomba vibali kutoka mamlaka husika kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo na kufanya biashara ya kuuza gesia kwa matumizi ya magari hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio alisema kuwa, shirika hilo limepanga kujenga vituo vikubwa vitano vya kusambaza gesi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Dkt. Mataragio aliweka wazi kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/21, TPDC imetenga kiasi cha shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vikubwa viwili Dar es Salaam ambapo kimoja kitakuwa kwa matumizi ya kujazia gesi asilia katika mabasi yaendayo kasi ya kampuni ya DART na kingine kitatumika kwa matumizi ya magari binafsi.

Sambamba na hilo, vituo vidogo viwili vya kujazia gesi asilia kwenye magari vitajengwa maeneo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Soko kuu la samaki Feri na kituo kimoja kwa ajili ya kupeleka gesi asilia katika Kiwanda cha Madawa cha Kairuki Kibaha.

Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani alitoa siku 10 kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Mtwara, kukamilisha kazi ya matengenezo ya Mitambo miwili ya kuzalisha umeme iliyoharibika katika kituo hicho kabla ya kuwaondoa kazini kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Mitambo minne ya kuzalisha umeme katika kituo hicho iliharibika hivi karibuni na kusababisha Mkoa wa Mtwara kupata tatizo la ukosefu wa umeme kwa muda mrefu, hata hivyo tayari mitambo miwili imeshatengenezwa na kurejesha huduma ya umeme. 

Aidha alitoa siku mbili kwa watendaji hao, kuunganisha mitambo miwili mpya iliyofungwa kituoni hapo katika mfumo unaotumia teknolojia ya Kisasa kuendesha mitambo hiyo ili kubaini kwa haraka tatizo linapotokea, badala ya mfumo wa kizamani unatumika sasa.

Aidha TANESCO wawe na utaratibu wa kufundishana na kupata mafunzo ya mara kwa mara juu ya ukarabati wa mitambo badala ya kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi.

“Tanesco mnauzofu wa miaka mingi katika kukarabati mitambo hii, rithishaneni utaalam, mkurugenzi awape mafunzo ya mara kwa mara, msitegemee watalaamu kutoka nje wanatuchelewesha, sababu ukimuhitaji leo kama anamambo yake hawezi kuja kwa wakati, najua uwezo huo mnao”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Na katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme alitoa miezi mitatu kwa TANESCO kufungwa vifaa maalum katika njia za kusafirisha umeme nchi nzima, vinavyofanya kazi ya kidhibiti hitilafu ya umeme inapotokea isiathiri eneo jingine.

Vifaa hivyo huimarisha hali ya umeme na endapo hitilafu itatokea eneo A, haiwezi kuathiri eneo B, pia itarahisisha kubaini eneo la tatizo katika eneo lililoathirika pasipo kuzima umeme katika eneo lote.

Alitoa agizo kuwa vifaa hivyo vitengenezwe na viwanda vya ndani na kununulia hapa nchini na ni marifuku kuagiza kutoka nje ya nchi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com