Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika mazishi ya mfanyabiashara maarufu Mkoani Lindi, Ally Nalaga yaliyofanyika katika kijiji cha Mnazimmoja mkoani humo, Februari 22, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mchinga, Mudihir Mudhiir (kulia) baada ya kushiriki katika mazishi ya mfanyabiashara maarufu mkoani Lindi, Ally Nalaga yaliyofanyika katika kijiji cha Mnazimmoja mkoani humo, Februari 22, 2021. Wa pili kulia ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika mazishi ya mfanyabiashara maarufu mkoani Lindi, Ally Nalaga yaliyofanyika katika kijiji cha Mnazimmoja mkoani humo, Februari 22, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wendelee kushikamana katika kipindi hiki ambacho dunia inamahangaiko makubwa na magonjwa mbalimbali ya maambukizi.
”Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu kama Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyotusisistiza na tuendelee kuiamini Serikali na jitihada za viongozi wake tutapata utulivu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 22, 2021) wakati aliposhiriki mazishi ya mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Lindi na Mtwara Ally Nalaga yaliyofanyika Mnazimmoja Lindi.
Amesema magonjwa hayo yameleta tafsiri tofaiti na wakati mwingine kutokuwa na utulivu kwani watu wanatishana sana na hali ambayo inawafanya wasiwe na amani na kuwajengea hofu.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa aina zote za magonjwa ambayo yanawakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini na kuyatafutia tiba.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya kila ugonjwa. ”Ukisikia ukimwi kuna tahadhari zake, ukisikia kipindupindi kina tahadhari zake.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini zote nchini waendelee kuliombea Taifa na viongozi ili liendelee kuwa na amani na kimbilio kwa walipoteza amani.
Akimzungumzia marehemu Nalaga, Waziri Mkuu amesema alikuwa mcheshi na mwenye upendo kwa kila mtu na alijitoa sana katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii.
”Tumepoteza mtu muhimu kwenye jamii yetu ya Wana Lindi na Mtwara. Bwana Nalaga ametuachia mambo mengi hivyo tumuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema.”
Waziri Mkuu amewaasa wananchi wayaenzi mambo yote mema aliyoyafanya enzi za uhai wake ikiwa ni pamoja na kujitoa katika shughuli za maendeleo ya jamii.
0 comments:
Post a Comment