METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, January 26, 2021

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUWA NA MABARAZA YA WAFANYAKAZI



NA SALEH RAMADHANI.

NAIBU Waziri wa Maji Marry prisca Mahundi mewataka wafanyakazi  wa Mamlaka ya udhibiti  wa huduma za Maji na Nishati Nchini(EWURA) kuhakikisha wanafahamu wajibu wao mahali pa kazi,ili kutekeleza malengo waliyopangiwa ya kutoa huduma kwa jamii katika muda uliopangwa.


Mahundi ameyasema hayo Januari 26,2021 Jijini Dodoma wakati akizindua baraza la Wafanyakazi wa EWURA ambapo amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati, kuondoa uzembe, rushwa na vitendo vyote visivyofaa mahala pa kazi ikienda sambamba na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija .


Amesema kuwa ni muhimu kwa Taasisi za umma kuwa na Mabaraza ya wafanyakazi kwani mabaraza hayo yameanzishwa kisheria kwa dhumuni la kuishauri Serikali katika ngazi za idara, Taasisi na Wizara kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali watu.


“EWURA mmefanya jambo jema kuanzisha tawi la TUGHE ambapo hali hii itasaidia utekelezaji wa majukumu, kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi, maslahi ya Wafanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi,”alisema Naibu waziri huyo wa Maji.


Sambamba na hilo  ametumia nafasi hiyo kuwataka wajumbe wa baraza hilo kuwa mfano wa kuigwa katika suala zima la uwajibikaji ili kuleta ufanisi kwani Uwajibikaji, ambayo ni nguzo kuu ya Mafanikio katika sehemu yoyote ya kazi ikiwa ni pamoja na   kutoa ushirikiano kwa watumishi ili kuondoa malalamiko na  kushughulikia masuala ya maendeleo kwa wakati.


Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa Baraza la Wafanyakazi ndilo jukwaa la kisheria la majadiliano ya pamoja, kati ya viongozi na watumishi katika utumishi wa umma kuhusu wajibu na maslahi ya watumishi .


Uundwaji wa baraza la wafanyakazi ni agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mwaka 1970, na ni utekelezaji wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 Kifungu 73(1-3) kinachoelekeza juu ya kutekeleza Sera ya kuwashirikisha Wafanyakazi katika uongozi wa pamoja kwa maana hiyo jambo hili ni jambo jema kwani linatambulika serikalini,”alisisitiza.

 

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) mkoa wa Dodoma,Nsubisi Mwasandende aliwataka wafanyakazi ambao hawajajiunga na chama hicho kujiunga kwa lengo la kuongeza nguvu ya Chama hicho ikiwa ni pamoja na kupata sehemu ya kutolea maoni yao.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com