Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akiongea na watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Michezo ambapo amewaagiza kukutana na Wadau wa sekta ya michezo nchini yakiwemo Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kubadilishana utaalamu wa namna ya kuendesha michezo kwa pamoja hatua inayosaidia taifa kusonga mbele kimichezo kitaifa na kimataifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Dkt. Hassan Abbasi ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini kukutana na Wadau wa sekta
hiyo wakiwemo Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kubadilishana utaalamu wa
namna ya kuendesha michezo kwa pamoja na kutoa ushauri wa kisera kwa wadau hao.
Dkt. Abbasi ametoa maagizo hayo leo Novemba 21, 2020 Jijini
Dodoma katika kikao watumishi wa Idara hiyo ambapo amewataka kusimamia
kikamilifu Sekta ya Michezo ambayo inaendelea kuletea heshima Taifa.
"Ni lazima mkutane na Wadau wenu ili mjue wana mawazo
gani katika sekta hii na nyie mtoe ushauri wa kitaalamu ambao utaleta tija. Ni
lazima muwaeleze wadau Sera ya Michezo inasemaje kwa sababu nyie ndio
mnaoisimamia sekta hii ", alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameitaka Idara hiyo kuhakikisha
kila Shirikisho au Chama cha michezo vinawasilisha Mpango Mkakati wake katika
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambao pamoja na mambo mengine, utaonyesha
kalenda ya mwaka katika ligi za kitaifa, kimataifa pamoja na timu ya Taifa .
Lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwepo na uelewa wa pamoja kwa wadau wote
utakaoleta mafanikio zaidi katika sekta hiyo.
Dkt. Abbasi amesema kuwa Taifa lazima liwe na ushiriki wa
mashindano ya michezo ambao utaleta tija, hivyo Idara hiyo ina jukumu la
kuhakikisha mashindano yote ambayo nchi inashiriki katika ngazi mbalimbali yanakua na
manufaa, ameongeza kuwa katika
mashindano mbalimbali ikiwemo Olympiki
lazima kama nchi kujua aina ya michezo ya kushiriki.
Vilevile, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ni mashindano ambayo
yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanazalisha vipaji vingi vya michezo
mbalimbali nchini. Hivyo, Idara ya Michezo ina jukumu la kusimamia mashindano
hayo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Elimu ili
vijana wanaofanya vizuri waendelezwe kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo
Malya pamoja na sehemu nyingine.
Kwa upande mwingine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa
ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta ya Michezo
unaendelea kuimarika ikiwemo kuimarisha Kombe la Mapinduzi.
"Muungano wetu ni muhimu na Kombe la Mapinduzi ni moja
ya njia ya kutuunganisha na kuimarisha Muungano wetu, hivyo nitoe rai kwa
Vilabu kupeleka timu bora katika mashindano hayo"alisema Dkt.Abbasi.
Akiongelea kuhusu miuondombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa
viwanja, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza na matarajio ni
kuwa na viwanja bora vya michezo nchini
na tayari Ujenzi wa Uwanja wa Dodoma
umefikia hatua nzuri.
0 comments:
Post a Comment