METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, October 4, 2020

SERIKALI: TUMEWEKA MAZINGIRA WEZESHI UTENDAJI WA NGOs NCHINI

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Vickness Mayao ambaye pia ni Msajili wa NGOs akizungumza wakati wa ufunguzi wa Ofisi ndogo za Shirika la Foundation For Civil Society mkoani Dodoma.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Vickness Mayao ambaye pia ni Msajili wa NGOs akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Ofisi ndogo za Shirika la Foundation For Civil Society mkoani Dodoma.

Serikali imesema imeweka mazingira wezeshi ya utendaji wa Mashirika Yasiyo ya kiserikali nchini zikiwemo Sheria, Kanuni, miongozo na taratibu mbalimbali zitakazowezesha kuwa na uratibu na usimamizi mzuri.

 

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Vickness Mayao wakati akifungua Ofisi ndogo za Shirika la Foundation For Civil Society mkoani Dodoma.

 

Aidha, Vickness amesema pamoja na kuyawekea Mashirika mazingira wezeshi, Serikali kwa kushirikiana na wadau imepitisha mwongozo wa uratibu wa pamoja wa Mashirika hayo na kupitia mwongozo huo Mashirika sasa yanaelekezwa kushirikiana na Sekta mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuzingatia vigezo vya kitaalamu. 

 

Vickness ametoa rai kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali pamoja na wadau wengine kutumia fursa ya kufungua Ofisi katika Makao Makuu ya nchi vizuri kwa maslahi ya mapana ya nchi yetu na maendeleo ya Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. 

 

Ameongeza kuwa amefurahishwa na Shirika hilo kwa kufungua Ofisi hiyo ambayo pia itatumika kama kituo cha Asasi za Kiraia jijini Dodoma na kitatumika kama kituo cha taarifa, ushauri, maarifa na mahali pa kufanyia kazi kwa wadau mbalimbali wakiwemo wadau wa maendeleo, wana Azaki, Asasi za kijamii, Serikali, sekta binafsi, Taasisi za kitaaluma na utafiti pamoja na jumuiya za kimataifa ili kuwezesha wananchi kupata, kutumia na kujifunza shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.

 

"Napenda kuchukua nafasi hii kulipongeza Shirika la Foundation For civil Society na Mashirika mengine yaliyoona umuhimu wa kufungua Ofisi zake hapa Dodoma" alisema

 

"Hili litatekelezwa vizuri endapo Mashirika yatapata fursa ya kupata taarifa sahihi na maarifa kupitia vituo vya kutoa taarifa kama hiki" alisema  

 

Pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha ushirikiano, uwazi na uwajibikaji na kujengeana uwezo kati ya Mashirika Yasiyo ya kiserikali ili kufikia maendeleo endelevu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com