METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, August 15, 2020

Jitihada za wadau zaongeza Uzalishaji wa Korosho ghafi nchini - Waziri Hasunga

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano Mkuu Mkuu Mkuu wa Korosho Mkoani Lindi tarehe 15 Agosti 2020. (Picha Na Innocent Natai) 

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akimkabidhi kitambulisho mkulima bora wa zao la Korosho wakati wa ufunguzi wa mkutano Mkuu wa Wadau wa Korosho mkoani Lindi.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Byakanwa (Kushoto) na Mhe Christina Mndeme Mkuu wa mkoa wa Ruvuma(Kulia) wakufuatilia hotuba wa Waziri wa Kilimo katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wadau wa Korosho

Na Innocent Natai, Lindi

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa uzalishaji wa zao la Korosho nchini umeongezeka jambo ambalo linaifanya serikali kuendelea kunufaika na uzalishaji huo mbali na kuwakomboa Wakulima.

Akizungumza na wadau wa Korosho katika Mkutano Mkuu wa wadau wa Korosho Waziri Hasunga amesema kuwa Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (Mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2019/2020), uzalishaji wa korosho ghafi nchini umeongezeka kutoka tani 155,244.645 hadi tani 313,826.386 sawa na ongezeko la asilimia 102%.

Pia, Ongezeko hili limeenda sambamba na ongezeko la fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani (USD) 185,000,000 mwaka 2015/2016 hadi USD 585,100,000 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 216%. Katika msimu 2018/2019 thamani ya mauzo nje ya nchi yalikua USD 196,500,000.

Hasunga ameongeza kuwa yapo mambo mbalimbali yaliyopelekea uzalishaji huo kuongezeka ikiwemo maboresho mbalimbali ya Usambazaji wa pembejeo kwa kuzingatia hali ya mahitaji ambapo kwa msimu uliopita,  usambazaji wa pembejeo ulihusisha Bodi ya Korosho na Sekta binafsi.

Aidha, amesema Kutokana na uwezo mdogo wa wakulima kununua pembejeo za korosho, Bodi ya Korosho ilikopesha pembejeo hizo ambazo malipo yake yalitakiwa kufanyika baada ya wakulima kuuza korosho zao za msimu wa 2019/2020. Jumla ya tani 34,152 zilisambazwa ambapo tani 8.610 za salfa ya unga zilinunuliwa na lita za maji 967,088 zilisambazwa ambapo lita 339,009 za viuatilifu vya maji ziliuzwa katika msimu husika.  

Amebainisha kuwa, Kutokana na mabadiliko ya mfumo wa manunuzi katika msimu wa 2020/2021 Serikali iliagiza pembejeo za korosho na vifungashio (magunia) vya korosho vinunuliwe na kusambazwa na Vyama vikuu vya Ushirika kwa kuzingatia mahitaji ya uzalishaji. Vyama vikuu tayari vinaendelea kukopesha pembejeo hizo kwa wakulima ambavyo vinatarajiwa kulipwa katika mauzo ya mwaka 2020/2021.

Amesema kuwa kutokana na mafanikio hayo kumekuwa na baadhi ya changamoto ikiwemo tija ndogo ya uzalishaji korosho, Ukosefu wa mbinu bora za kilimo cha korosho ikiwemo; matumizi madogo na yasiyo sahihi ya pembejeo, wakulima wengi bado wanaendeleza kilimo cha kutumia mikorosho ya asili ambayo hutoa korosho chini ya kilo 10 kwa mti mmoja tofauti na matarajio ya uzalishaji wa zaidi ya kilo 20 kwa mti kwa mwaka, mikorosho zaidi ya asilimia themanini (80%) imezeeka na hivyo kupoteza uwezo wa kutoa mazao kulingana na matarajio. "Hayo yote yanachangia katika kuongeza gharama za uzalishaji na kupunguza faida ambayo mkulima angeweza kuipata" Amekaririwa Waziri Hasunga

Sambamba na hayo Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema kuwa Wizara ya Kilimo imepanga kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kutoka tani 300,000 hadi 1,000,000 kwa mwaka ifikapo 2023/2024. Katika kutekeleza hayo, Wizara imepanga kuimarisha Tasnia ya Korosho nchini kwa kuboresha usimamizi, Kuongeza uzalishaji na tija, kuongeza thamani ya korosho na kuimarisha mfumo wa masoko kupitia mikakati mbalimbali.

Mkutano Mkuu wa Wadau wa Korosho hufanyika mara moja kwa mwaka na hujumuisha wadau mbalimbali wa Korosho hususani wakulima na wengine wanaoshiriki moja kwa moja katika mnyororo mzima wa Kilimo cha Korosho ambapo mwaka huu umefanyikia Mkoani Lindi huku Mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga

MWISHO


Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com