Nyumba za walimu (sita katika moja) zilizopo katika shule ya Sekondari ya kutwa ya Sawe iliyopo katika Kijiji cha Saawe, Kata ya Masama Mashariki, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
SERIKALI
imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Sekta ya elimu na mafunzo, kwa mujibu wa
Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya
Taifa 2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya
rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na
kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye
uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025.
Serikali
iliandaa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ili kutoa mwelekeo wa
elimu na mafunzo nchini kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii,
kisayansi na kiteknolojia na changamoto za elimu na mafunzo kitaifa, kikanda na
kimataifa, ili kuongeza fursa, ufanisi na ubora wa elimu na mafunzo nchini na
kufikia viwango vya rasilimaliwatu kwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025.
Sera
hii imeweka Dira ya elimu na mafunzo nchini kuwa ni “Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na
mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa” na
Dhima yetu kuwa ni “kuinua ubora wa elimu
na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya
Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia
katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu”.
Akifungua rasmi Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, jijini Dodoma, Novemba 20, 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe magufuli pamoja na mambo mengine alisema, juhudi
kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo
vikuu.
Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na
kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi. Aidha, Serikali itahakikisha kwamba
vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara,
vitabu, madawati, n.k.
Aliweka bayana kwamba Serikali itahakikisha kuanzia
Januari 2016 elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure.
“Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa
wakati. Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja
na kujenga nyumba za walimu vijijini” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza
mwezi Juni mwaka huu, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi
wa Chama cha Walimu (CWT), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli alisema kuwa moja ya
vipaumbele vya Serikali yake ni kukuza na kuimarisha Sekta ya elimu nchini,
na kuwa Serikali itaiendeleza sekta hiyo
hususan katika kupanua wigo na kuboresha elimu inayotolewa kuanzia ngazi ya
awali hadi elimu ya juu, sambamba na kuendelea kuajiri walimu .
Ni
dhahiri shahiri kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutekeleza sera hiyo
ya elimu nchini kwa kufanya mapinduzi yanayolenga kuzalisha wasomi na watendaji
watakao iendeleza Tanzania ya viwanda na nchi yenye uchumi ulioimarika zaidi.
Mapinduzi
hayo yanajidhihirisha katika maboresho ya sekta hiyo ambapo shule ya Sekondari
ya kutwa iliyopo katika Kijiji cha Saawe, Kata ya Masama Mashariki, Wilaya ya
Hai mkoani Kilimanjaro imenufaika kupitia utekelezaji unaofanywa na Serikali wa
kuboresha nyumba za walimu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Mradi
wa ujenzi wa nyumba za walimu sita ndani ya moja (six in one) katika Shule ya
Sekondari Sawe yenye jumla ya wanafunzi 213 unatajwa kuboresha mazingira ya
kuishi walimu na kuongeza ufanisi wa kazi ya kufundishia.
Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Sekondari Sawe, Gaudence Silayo anasema kuwa shule hiyo
ilipoanza mwaka 2007 haikuwa na nyumba za walimu, badala yake walimu waliishi
mitaani katika nyumba za kupanga na kutokana na hali ya hewa iliyopo katika
eneo hilo ya mvua nyingi na matope walimu walipata shida na walifika shuleni
kwa kuchelewa jambo ambalo lilishusha
kwa kiwango kikubwa ufaulu wa shule
hiyo.
“Mradi
huu wa ujenzi wa nyumba sita katika moja ulipokuja kwa bajeti ya mwaka
2015/2016 wenye gharama ya shilingi 150,586,100 ambao ulikamilika mwaka 2017,
basi kuanzia wakati huo walimu sita waliweza kuishi hapa shuleni, jambo hilo
lilileta faraja na matumaini makubwa na liliongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa
walimu” anasema Mwalimu Silayo
Aidha,
akifafanua faida za kuwepo kwa nyumba hizo, mwalimu Silayo anasema kuwa shule
iliandaa masomo ya ziada baada ya masomo ya darasani ambapo wanafunzi walifaulu
vizuri, kidato cha pili walifaulu wote isipokuwa mwanafunzi mmoja na wanafunzi
wa kidato cha nne walifaulu wote isipokuwa wanafunzi watatu.
Naye,
mwalimu Germana Mtenga anayefundisha katika shule hiyo anasema kuwa faida ya
kuwa na nyumba zinatoa fursa kwa walimu kutoa msaada wa masomo wa ziada kwa kwa
wanafunzi hasa kwa sababu tayari walimu wamekuwa na utulivu, sambamba na
kuwasaidia wanafunzi wa kike wanapokuwa wamepata matatizo mbalimbali.
Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imejipambanua
kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kutoa elimu bila malipo katika shule za
msingi na sekondari, tangu Disemba, 2015 hadi Februari, 2020 imetumia jumla ya
shilingi Trilioni 1.01/=. Maboresho mengine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule za Msingi kutoka 16,899
zilizokuwepo mwaka 2015 hadi shule 17,804 mwaka 2020. Shule za Sekondari nazo
zimeongezeka kutoka 4,708 hadi 5,330 mwaka 2020.
Fauku ya hayo, ukarabati wa shule kongwe za
Sekondari 73 kati ya shule Kongwe 89, kujengwa mabweni 253 na nyumba za walimu
na maabara 227, Serikali imetoa vifaa vya maabara vipatavyo 2,956 na kupunguza
tatizo la uhaba wa madawati kutoka madawati 3,024,311 mwaka 2015 hadi
madawati 8,095,207 mwaka 2020.
Vilevile bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu imeongezeka kutoka shilingi bilioni 341 kwa mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 450 mwaka 2019/2020.
0 comments:
Post a Comment