Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akipewa maelezo kutoka kwa Mhandisi Mkuu Msaidizi wa Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi cha Mgololo, Gregory Chogo wakati alipotembelea jana Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi Mgololo ( MPM) kwa lengo la kujua changamoto wanazokabiliana nazo wakati wanapohitaji Malighafi kutoka katika Shamba la Miti la Sao Hill lililopo wilaya ya Mufindi katika mkoa wa Iringa. Kulia ni Katibu Tawala wa wilaya ya Mufindi, Endrew Musimbwa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akiwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Mufindi pamoja na Watumishi wa Shamba la Miti Sao Hill akizungumza na Mwekezaji wa Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi Mgololo, Kashamiri, Shamir ( wa tatu kushoto) mara baada ya kutembelea kiwanda hicho ikiwa lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na Wanunuzi wakubwa wa Malighafi kutoka katika Shamba la Miti la Sao Hill.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amekutana na kufanya mazungumzo Wanunuzi Wakubwa wenye viwanda wanaonunua malighafi inayozalishwa kutoka katika Shamba la Miti Sao Hill lililopo katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Akizungumza jana mkoani Iringa kwa nyakati tofauti na Uongozi wa Wamiliki wa Viwanda hivyo, Mhe.Kanyasu amesema lengo la ziara hiyo ni kutaka kujua changamoto wanazokabiliana nazo wakati wanapohitaji malighafi hizo ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi na kujua jinsi gani mlipuko wa virusi vya Corona ulivyoathiri katika Uzalishaji wao.
Katika ziara hiyo, Mhe.Kanyasu alitembelea Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi cha Mgololo ( MPM) na Kiwanda cha Kuzalish nguzo za Umeme (Mufindi Woodpoles and Timber LTD)
" Nimeamua kufanya ziara hii ili kuweza kukutana na Wawekezaji ambao ni wateja wakubwa wa shamba hili, Kama Wizara tumeona ni muhimu wa kuwatembelea ili kuweza kuwasikiliza na endapo kama wana changamoto ziweze kushughulikiwa haraka" alisisitiza Mhe.Kanyasu.
Akizungumza na Wanunuzi hao kwa nyakati tofauti, Wanunuzi hao wamemueleza kuwa wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill pindi wanapohitaji Malighafi kwa ajili ya Viwanda vyao bila vikwazo vyovyote.
" Mimi kama Waziri mwenye dhamana nimefarijika sana kusikia kutoka kwa Wanunuzi hawa kuwa wamekuwa hawapati changamoto yoyote wakati wanapohitaji Malighafi kutoka Shamba la Miti Sao Hill" alisema Kanyasu
Aidha, Mhe.Kanyasu amesema ziara hiyo imekuwa muhimu kwa sababu imetoa nafasi kwa Serikali kujitathmini na pia imewapa nafasi Wateja wa Shamba hilo kusema hisia zao kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Muuzaji na Wanunuzi wa Malighafi za mazao ya Misitu.
Katika hatua nyingine Mhe.Kanyasu amesema ugonjwa wa Corona umewaathiri kwa kiasi Wazalishaji hao licha ya kuwa waliendelea na uzalishaji kama kawaida lakini bidhaa zao hazikuweza kusafirishwa kwenda nchi za nje kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka yao.
Kwa upande wake Mhandisi Mkuu Msaidizi wa Kiwanda cha Kuzalisha Karatasi cha Mgololo, Gregory Chogo amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kuonesha kuwathamini na kuwajali wateja wa Shamba hilo kwa kuamua kuwatembelea baadala ya kusubiri kuletewa taarifa mezani.
Amemuhakikishia kuwa wataendelea kununua malighafi katika Shamba hilo kadri ya mahitaji kufuatia ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa Uongozi wa Shamba hilo na endapo kutakuwa na vikwazo hawasita kusema ili vitatuliwe.
Hata hivyo, Mhandisi Chogo amemueleza kuwa kwa sasa Kiwanda kimesimama uzalishaji kutokana na janga la Corona kwa sababu bidhaa zilizolishwa tayari hazijaanza kusafirishwa nchi za nje.
0 comments:
Post a Comment