Ni
majuzi Mzee wetu Mpendwa, Benjamin William Mkapa ukiwa Dodoma uliongoza Kikao
cha Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa umahiri mkubwa, kumbe ndo
ulikuwa ukituaga! Wengine tulijua kuwa utapiga kura Oktoba na kushiriki katika
sherehe za kumwapisha Rais atakayekuwa amechaguliwa, kumbe sivyo, Mkapa
umetutangulia ghafla kwenda kwa Muumba wetu. Burian Mzee wetu wa Uwazi na
Ukweli.
Tutakukumbuka
kwa uongozi wako uliotukuka na unyenyekevu uliokuwa nao kwa kuwaheshimu wakubwa
kwa wadogo tangu ukiwa Pugu Sekondari, Chuo Kikuu Makerere hata ulivyorudi
nchini na kuendelea na majukumu yako kwa uzalendo mkubwa. Kwenye Tasnia ya
Habari msiba huu ni pigo kwani Mzee Mkapa alikuwa Mhariri mahiri wa The Nationalist hadi Daily
News. Waliofanya nawe kazi akiwemo mwandishi nguli, Jenerali Ulimwengu
anasema kuwa kwenye chumba cha habari Mzee Mkapa alikuwa mwalimu na mlezi.
Mkapa
atakumbukwa kwa kupinga na kupambana na rushwa. Katika kudhihirisha hilo, Mzee
Mkapa aliunda Tume ya Warioba kuchunguza vitendo vya rushwa na kutoa
mapendekezo. Hakuishia hapo kwani aliunda Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU)
ambayo baadae ikaja kujulikana kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU).
Wakati
Mzee Mkapa anaingia madarakani alikuta uchumi wa nchi unayumba, hivyo alibuni
mbinu kadhaa za kufufua uchumi. Moja ya mbinu aliyoibuni kiongozi huyo ni
kuunda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kubuni vyanzo vya mapato na
kukusanya kodi.
Hakuishia
hapo bali alitilia mkazo ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na
kuboresha usafiri wa majini. Katika hili alianzisha Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS). Wakala ambao ulijenga barabara kwa kiwango cha lami za kuunganisha
mikoa yote ya Tanzania Bara. Kwenye hotuba zake za kila mwezi hakuchoka
kujinadi na kazi yake ya kuboresha miundombinu. Mzee Mkapa alisikika akisema,
“Tumeboresha miundombinu, tumejenga shule za msingi na sekondari”.
Mkapa
alifanikisha kuunda Taasisi za udhibiti, Taasisi na mifuko ya kuinua Wananchi
kama Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) na
Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
Jambo
jingine ambalo watanzania wanapaswa kulijua au kulikumbuka ni lile la kumuibua
Jemedari Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli alipomteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi chini Waziri
Anna Abdallah mwaka 1995.
Ukweli
na Uwazi ndio ilikuwa Kaulimbiu maarufu ya Mpendwa wetu Benjamin William Mkapa.
Aliamini kuendesha Serikali yake kwa ukweli na uwazi.
0 comments:
Post a Comment