Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kipindi cha 2015-2020 ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula ameibuka kidedea katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya CCM uliofanyika Jumatatu Julai 20, 2020 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa kupata idadi ya kura 502 dhidi ya wagombea wenzake.
Akitaja matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi Ndugu Sixtus Reuben amesema kuwa jumla ya wagombea katika uchaguzi huo walikuwa 71 na idadi ya wapiga kura ni 666 huku akimtangaza Mgombea huyo kama mshindi wa kura za maoni huku akifuatiwa na Ndugu Israel Joseph Mtambalike aliyepata idadi ya kura 112 na Mhandisi Ngilila Jonas Ngilila akipata kura 13 akishika nafasi ya tatu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa uchaguzi huo ambae pia ni katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula akawashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa ushirikiano walioutoa katika kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa uwazi, uhuru na haki huku akiwataka wagombea kuwa kitu kimoja na kuvunja makundi kwani mchakato wa uchaguzi haujaisha mpaka vikao vya uteuzi utakapokamilika.
Akihitimisha mshindi wa kura za maoni katika uchaguzi huo, Dkt Angeline Mabula akawashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kuendelea kumuamini na kumpa ridhaa ya kuendelea kutumikia jimbo hilo kama vikao vya uteuzi vitaridhia ili aweze kuungana na mgombea wa nafasi ya uraisi wa chama hicho Mhe Dkt John Magufuli katika kuwaletea maendeleo sanjari na kuahidi kuwatumikia kwa uadilifu mkubwa na nguvu zote kwa kipindi cha miaka mitano mingine ili kuendeleza yale mazuri waliokuwa wameanza kuyatekeleza.
0 comments:
Post a Comment