Mhudumu wa Afya Zahanati ya Madizini, Wilayani Mvomero Bi. Grace Ligombi akitakasa mikono kabla ya kuanza kutoa huduma za chanjo kwa watoto. Picha na Englibert Kayombo.
Mtoto Mustapha Pangani (14) akiwa amempeleka mdogo wake Ismail Pangani (Mwaka mmoja na nusu) kliniki katika Zahanati ya Madizini wakihojiwa na mwandishi mwandamizi wa Gazeti la JAMVI LA HABARI, Veronica Mrema. Picha na Englibert Kayombo.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Morogoro Bw. Abdulkadiri Kakai akikau jotoridi kwenye jokofu la kuhifadhi chanjo katika Zahanati ya Madizini Wilayani Mvomero.
WAZAZI na walezi wamehimizwa kuzingatia kuavaa barakoa kila
wanapowapeleka watoto wao hospitalini, vituo vya afya na zahanati kupatiwa
huduma mbalimbali za kiafya ikiwamo zile za chanjo.
Rai hiyo imetolewa leo Mkoani hapa na Ofisa Miradi kutoka
Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD), Dk. Furaha Kyesi alipozungumza na
wazazi na walezi waliofika katika Zahanati ya Madizini iliyopo Kata ya Mtibwa
Wilayani Mvomero kupata chanjo na kupima uzito wa watoto wao.
Maofisa wa Mpango huo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto wa Mkoa wa Morogoro na wa Manispaa wako katika ziara ya
kukagua utoaji huduma za chanjo katika Mkoa huo kwa kushirikiana na Shirika la
Engender Health kupitia Merck Sharp & Dohme B.V (MSD).
Dk. Kyesi amesema huduma za chanjo nchini hazijasitishwa
bado zinaendelea kutolewa kulingana na ratiba za watoto walizopangiwa na
kulingana na umri wao hata hivyo jambo la msingi ni kila mmoja kuhakikisha
anajikinga kila anapompeleka mtoto.
“Kila mmoja anapaswa kuvaa barakoa, jikinge ili uwakinge na
wengine kwa sababu hapa hakuna anayejua mwenzake ametoka wapi, amekutana na
nani hadi amefika hapa kwenye zahanati.
“Ukiwa umevaa barakoa inasaidia kukukinga lakini pia
unawakinga na wale wanaokuzunguka, vile vile mnapofika hapa kituoni zingatieni
kunawa mikono na kukaa umbali wa mita moja, hakikisha unapokaa mkono wako
ukiunyoosha hauwezi kugusa bega la mwenzako aliye pembeni yako,” amesisitiza
Dk. Kyesi.
Amesema ni muhimu pia mama kuzingatia kunawa au kutakasa
mikono kila anapohitaji kumnyonyesha mtoto wake ili aendelee kumkinga naye pia,
watoto wadogo hatushauri wavalishwe barakoa.
Awali, Muuguzi wa Zahanati hiyo, Eliainenyi Tarimo amesema
kila mwezi wamelenga kuwachanja watoto 34 lakini kwa kuwa jamii ina mwamko
mkubwa wa chanjo wamefanikiwa kuvuka lengo hilo na kuchanja watoto zaidi ya
100.
“Tunaendelea kutoa chanjo kwa kuzingatia mwongozo tuliopewa
na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa kujikinga
tusipate maambukizi.” Amesema Eliainenyi na kuendele kusema kuwa kabla ya mzazi au mlezi kuingia ndani ya
kituo hicho kwanza anatakiwa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ambapo
ndoo imewekwa katika eneo la kuingilia katika Zahanati hiyo.
Eliainenyi amesema awali utaratibu waliokuwa wakiutumia
kabla ya kuchukuliwa kwa tahadhari ya mlipuko wa Corona walikuwa hawana kabisa
utaratibu huo.
“Walikuwa tu wakifika wanakwenda moja kwa moja sehemu ya
kuweka kadi, wanakaa kwenye mabenchi na kusubiri kuitwa majina, tukaona tuanze
kuwapa namba na kuwaruhusu wakae kwa kupeana nafasi ya mita moja kwenye
mabenchi.
“Mabenchi tuliyonayo hayatoshelezi lakini eneo letu ni kubwa
hivyo wanakaa na hapo nje kwa kupeana nafasi, tunapomaliza kumhudumia mtoto,
tunawaomba waondoke mapema kwenda nyumbani na si kuendelea kukaa hapa,”
amesisitiza.
Amesema changamoto pekee inayowakabili sasa ni wazazi na
walezi hao kuwa na mwitikio mdogo wa uvaaji barakoa jambo ambalo hawachoki
kuwasisitiza na kuwahimiza kuzingatia ili kuendelea kujikinga.
Amesema kwa upande wa chanjo ya HPV ambayo hupatiwa
wasichana wenye umri wa miaka 14 iliyokuwa ikitolewa shuleni na kwa kuwa sasa
zimefungwa kutokana na mlipuko wa CORONA, hivi sasa zinaendelea kutolewa katika
Zahanati hiyo.
“Japo bado hatujawaona wengi wakija, wachache wameshakuja
tumewachanja, tunaendelea kuwahimiza waje kupitia watoa huduma za afya wa ngazi
ya jamii (CHW’s) na hapa kituoni huwa tunawaeleza wanajamii wanaokuja kliniki
kwamba waende wakawahimize wasichana waje kupata chanjo ya pili,” amesema.
0 comments:
Post a Comment