Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua vitalu vya miche bora ya zao la michikichi aina ya Tenera katika Gereza Kwitanga mkoa wa Kigoma leo
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akikagua kitalu cha miche bora ya zao la michikichi katika Gereza Kwitanga mkoa wa Kigoma leo alipotembelea kuona utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za michikichi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mche bora wa mchikichi uliozalishwa na Kituo cha utafiti TARI Kihinga mkoa wa Kigoma leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyeshika miche ) akikagua kitalu cha miche ya michikichi inayozalishwa na Gereza Kwitanga kwa ushirikiano na TARI Kihinga.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali (Mst.) Emanuel Maganga wa kwanza kushoto akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (katikati) mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Mkuu huyo wa mkoa kuhusu uendelezaji wa zao la mchikichi.Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Bw.Rashid Mchata.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo amewapongeza
watafiti wa mbegu za michikichi kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora na
kuwataka watumie muda mfupi zaidi wa kuzalisha
na kuzisambaza kwa wakulima nchini
Agizo hilo limetolewa leo mjini Kigoma na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerald Kusaya wakati alipotembelea kukagua kituo cha
Utafiti wa kilimo ( TARI) Kihinga, Gereza Kwitanga na JKT Bulombola zenye
jukumu la kuzalisha miche bora ya michikichi aina ya Tenera.
“ Watafiti endeleeni na utafiti wa kupunguza
muda wa kuzalisha mbegu bora toka miezi 18 hadi chini ya mwaka mmoja ili
wakulime wapate mbegu hizo kwa wingi waongeze uzalishaji kufikia lengo
lililowekwa la miche milioni tano kwa mwaka” alisema Kusaya
Kusaya alisema ametembelea mkoa wa Kigoma
kufanya ufuatiliaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilitoa mwezi
Agosti mwaka 2018 la kuitaka wizara ya kilimo kuzalisha miche bora ya
michikichi milioni 20 kwa kipindi cha miaka minne na kugawa kwenye halmashauri
za mkoa huo na mikoa mingine ili nchi ipate mafuta ya kutosha ya kula.
Katibu Mkuu huyo alisema ni lengo la serikali
kuona zao la michikichi linalimwa mikoa mingi zaidi na ili kukabiliana na
upungufu wa mafuta ya kula nchini kwani zao hilo ndio tegemeo kubwa la viwanda
vya mafuta..
Awali Kusaya alisema kwa sasa Tanzania inatumia
shilingi Bilioni 443 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi kutokana na
uzalishaji wa mazao ya mafuta kuwa mdogo .
“ Kwa mwaka nchi inahitaji mafuta ya kula tani
570,000 wakati uzalishaji wa ndani ni tani 250,000 sawa asilimia 36 hivyo kuwa na upungufu wa tani 220,000 “ alisema Katibu Mkuu huyo
Awali akiwasilisha taarifa ya Kituo cha TARI
Kihinga Mkurugenzi Mkuu wa TARI Geofrey Mkamilo alisema agizo la Waziri Mkuu
limeanza kutekelezwa kwani kufikia Mwezi Aprili mwaka 2020 jumla ya mbegu bora
za michikichi 1,791,768 ambazo zinaweza kupandwa kwenye eneo la ekari 35,835.
Dkt.Mkamilo aliongeza kusema jumla ya
mbegu za michikichi aina ya Tenera
1,255,111 na miche bora 167,315 imezalishwa na taasisi za umma na binafsi
kutekeleza agizo la Waziri Mkuu.Mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno tani 5
kwa hekta .
Nae Mkuu wa Gereza Kihinga SSP Dominic Kazmil
alimweleza Katibu Mkuu kuwa jumla ya mbegu 273,050 zimezalishwa tayari na miche
8,050 ipo tayari kwenda kupandwa na wakulima kwenye halmashauri za Mkoa wa
Kigoma .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia
Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru Wizara ya Kilimo kwa jitihada za kuhakikisha
mkoa wa Kigoma unakuwa kitovu cha uzalishaji miche ya zao la michikichi.
Katika ziara hii ya mkoa wa Kigoma Katibu Mkuu
Kusaya ameuomba uongozi wa mkoa kuhamasisha wakulima pamoja na kuzalisha
michikichi sasa waanze pia kuzalisha mazao kama mkonge na korosho ili kuongeza
wigo wa mapato kwenye mazao ya biashara.
Kusaya alisema ni wakati sasa wataalam wa
kilimo wakawaelimisha wakulima waongeze mazao mengine ya biashara kama korosho
na mkonge ili kuwa na uhakika wa kipato kwani ardhi ya Kigoma inafaa na kuwa
wizara yake ipo tayari kuleta mbegu bora za mkonge na korosho.
0 comments:
Post a Comment