Waziri wa
Nishati, Dkt.Medard Kalemani,( kulia) akiteta jambo na Mbunge wa Igalula, Musa
Ntimizi( kushoto), wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji
umeme vijijini na kuwasha umeme katika baadhi ya nyumba za wakazi wa Kijiji cha
Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, Mei 19,2020.
Waziri wa
Nishati, Dkt.Medard Kalemani, akiwaonyesha kifaa cha Umeme tayari (UMETA)
wakazi wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, alipofanya ziara ya
kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji hicho, Mei
19,2020.
Waziri wa
Nishati, Dkt.Medard Kalemani, akiwasha mashine ya kusaga na kukoboa nafaka
ambayo sasa inatumia umeme badala ya mafuta mazito kujiendesha, inayomilikiwa
na Mkazi wa Kijiji cha Loya wilayani Uyui Mkoani Tabora, wakati alipofanya
ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji
hicho, Mei 19, 2020.
Waziri wa
Nishati, Dkt.Medard Kalemani,(katikati), Mbunge wa Igalula, Musa Ntimizi na
Viongozi wengine walioambatana nao wakipita katika mitaa ya Kijiji cha Loya
wilayani Uyui Mkoani Tabora, walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya
usambazaji wa umeme vijijini, katika kijiji hicho,na kuwasha umeme Mei 19,2020.
Wakazi wa
Kijiji cha Loya wilayani Uyui mkoani Tabora, wameishukuru Serikali kupitia
Wizara ya Nishati kwa kuwaunganisha na kuwawashia umeme katika kijiji hicho
ambacho awali wakazi hao walikuwa wakiona kama ni ndoto.
Wakazi hao,
wameeleza hayo baaada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuwasha umeme
katika kijiji hicho na kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika
wilaya hiyo, Mei 19, 2020.
Wakazi wa
Kijiji hicho walisema kuwa, miaka mingi wamekuwa wakipewa ahadi
zisizotekelezeka na wakati mwingine wamekuwa wakikatishwa tamaa ya kupata umeme
kwa kuwa kijiji hicho kiko umbali mrefu kutoka ilipo miundombinu ya umeme pia
kuwa na jiografia isiyorafiki kufika maeneo hayo.
“Huyu
Waziri ameandika historia hapa Loya, haijawahi kutokea kiongozi mkubwa ngazi ya
Waziri kufika katika kijiji chetu tangu kimeanzishwa, wengi wanakuja katika
wilaya hii lakini wanaishia huko mujini tu vijijini hawafiki, na amekuja
kutuwashia umeme kabisa kwakweli tunamshukuru sana huyu Dkt. Kalemani, pia
tunamshukuru Rais Magufuli kumkubalia huyu waziri kuja huku kwetu kutuletea
umeme, abarikiwe sana”, alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Josephat
Wamalulu.
Kwa upande
wake Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani alisema baada ya kusikia malalamiko
na kuona uhitaji mkubwa wa umeme kwa kijiji hicho ambapo bado hakijafikiwa na
mradi wa kusambaza umeme (REA) kwa kipindi hiki,nililiagiza Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO) kupeleka umeme kwa gharama zao katika kijiji hicho.
Alisema
kijiji cha Loya kinawakulima wengi wa mpunga, karanga na wafanyabiashara ambao
wanahitaji huduma ya umeme katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Kwa mantiki
hiyo, TANESCO ilitenga zaidi ya shilingi Bilioni 3 ili kuhakikisha umeme
unafika katika kijiji hicho, ambacho kiko umbali mrefu sana kutoka ilipopita
miundombinu ya umeme.
“Niliwaagiza
TANESCO kuleta umeme hapa Loya,kama mlivyoona Loya inawakazi wengi wakulima na
wafanyabiashara ambao wanahitaji umeme katika shughuli zao, tumetenga zaidi ya
shilingi Bilioni tatu kuhakikisha umeme unafika hapa na tutapeleka katika
vijiji vingine cha msingi hapa ni ninyi wananchi kusuka nyaya katika nyumba
zenu, na kulipia shilingi 27,000 tu umeme utawafikia”, alisema Dkt. Kalemani.
Aidha
aliwaagiza TANESCO, kuendelea kusambaza na kuwawasha umeme kwa wakazi wa eneo
hilo waliokwisha kulipia gharama za kuunganishiwa umeme ndani ya siku 7 baada
ya kulipia.
Aliwataka
wakazi wa Loya kutumia umeme huo kujiendeleza kiuchumi badala ya kuutumia umeme
huo kwa kuwasha taa peke yake.
Kwa upande
wake Mbunge wa Jimbo la Igalula, Musa Ntimizi aliwataka wafanyabiashara katika
kijiji hicho kutanua wigo wa kibiashara na wakulima wa mpunga kuongeza thamani
ya mazao yao ili kupata faida zaidi.
Pia wakazi
hao wachangamkie fursa hiyo ya umeme kwa kuazisha biashara na viwanda vidogo
vinavyotumia umeme, kama vile Saloni, Mashine za kusaga na kukoboa nafaka,
kuchomelea vyuma na kadhalika.
“Umeme huu
umekuja wakati muafaka kwa wakazi wa Loya, sasa hivi tutaanza kuuza mchele safi
na bora badala ya mpunga ambao hata hivyo wafanyabiashara kutoka nje ya hapa
walikuwa wakiwalangua kwa wakulima wa eneo hili, sasa hivi kutakuwa na mashine
za kisasa za kukoboa mpunga na wakulima wataongeza thamani ya mazao yao na
kunufaika zaidi na kilimo cha mpunga”, alisema Ntimizi.
Aliwaeleza
wakazi hao kuwa wasikubali kuuziwa nguzo za umeme, pia watumie wakandarasi
walioidhinishwa na TANESCO kufanya kazi ya kutandaza nyaya katika nyumba zao
ili kuepuka vishoka.
0 comments:
Post a Comment