METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, May 30, 2020

BARAZA LA MADIWANI LA KAWAIDA, ROBO YA TATU 2019/2020 LAKETI MUSOMA DC, MIKOPO, MAPATO, HATI SAFI NA MIRADI YA MAENDELEO YATIA FORA





Alhamisi 28 Mei, 2020, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma imefanya Baraza la kawaida la  Madiwani la robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2019/2020 katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mugango.

Baraza hilo limehudhuliwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh. Charles Nyambita, Mkurugenzi Ndg. John Lipesi Kayombo, Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo, viongozi wa vyama vya siasa, wadau mbalimbali pamoja na  wananchi

Akizungumza wakati wa Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma  Mh. Charles Nyambita alimpongeza Mkurugenzi, Madiwani  pamoja na wataalamu wa Halmashauri hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii jambo lililopelekea Halmashauri hiyo kupata hati safi kwa mwaka wa nne mfululizo.

"Kwa mwaka wa nne mfululizo Halmashauri yetu imepata hati safi hili ni jambo la kipekee sana, hongera sana Mkurugenzi, Madiwani na wataalamu kwa kufanikisha hili, hata Waheshimiwa Madiwani mnapoenda kunadi sera na kusema hili kunakuwa hakuna maswali kutoka kwa wananchi "  alisema Mh. Nyambita.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Ndg. John Lipesi Kayombo alisema Halmashauri hiyo mpaka sasa ipo katika hatua nzuri katika ukusanyaji wa mapato, utoaji wa asilimia 10 za mikopo, utoaji wa asilimia 20 za mapato ya kila Kijiji na miradi ya maendeleo.

"Mheshimiwa Mwenyekiti mwaka 2018/2019 tulikusanya mapato zaidi ya 100%, mwaka huu 2019/2020 mpaka mwezi wa nne tumeshakusanya 91.4%, tunaamini mpaka mwaka huu wa fedha utakapoisha tutakusanya zaidi ya 100%.

"Upande wa utoaji wa 20% ya fedha ya makusanyo ya kila Kijiji mpaka sasa tumeshapeleka 100% ya kiasi hicho cha fedha kwenye kila Kijiji.

"Kwenye 10% ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Walemavu mpaka kufikia mwezi wa tatu mwaka huu tulikuwa tumeshapeleka 90% ya Mikopo hiyo, lengo ni mpaka kufikia mwezi wa sita tuwe tumezidi 100% ya utoaji wa mikopo hiyo".

"Mafanikio haya yote yamekuja kutokana na upendo, umoja na mshikamano  uliopo kati yangu, Baraza la Madiwani, wadau mbalimbali, kufanya kazi kwa weledi, kushirikiana na wakuu wa idara na vitengo na usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi yake, ikumbukwe kwamba halmashauri hii ilikuwa  haijawahi kufikisha asilimia 100 ya ukusanyaji wa mapato tangu kuanzishwa kwake ila kwa sasa  tunakusanya na kuvuka 100% ya mapato ya ndani "alisema Kayombo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com