METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, April 26, 2020

KUSAYA,VIJANA JIFUNZENI KILIMO BIASHARA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua kitalu nyumba kilichopandwa nyanya na vijana walliopo katika Kituo Atamizi cha Vijana kujifunza Kilimobiashara chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mjini Morogoro.
Kijana Hefsida Olloo (Kushoto)akitoa maelezo ya nanma alivyofanikiwa kuzalisha nyanya katika kitalu kwenye kambi Atamizi ya SUA .Hefsida ni mhitimu wa Shahada ya Sayansi katika Hisabati toka Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2018 aliyeamua kufanya kilimo biashara.Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya alipotembelea chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine hivi karibuni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika hoho za rangi zinazozalishwa na vijana katika kituoo atamizi cha mafunzo kwa vitendo chini ya SUA.Kulia kwake ni Msimamizi wa kituo hicho Zebedayo Sanga na kushoto kwake ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Prof.Raphael Chibunda.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua kitalu kinachozalisha hoho za rangi katika kituo atamizi cha vijana kujifunza kilimobiashara chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine mjini Morogoro hivi karibuni.Jumla ya vjana wahitimu wa kozi mbalimbali wapatao 40 wanapata mafunzo kwa mwaka mmoja kwenye kituo hicho .
Sehemu ya vijana wanaopata mafunzo kwa vitendo katika kituo atamizi  Chuo Kikuu cha Sokoine kujifunza kilimobiashara wakimsikiliza Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (hayupo pichani) wakati alipowatembelea hivi karibuni mjini Morogoro.

Vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini wameshauriwa kujitokeza na kupata mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara kwa ajili ya kujipatia ujuzi na ajira toka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine.

Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati akiongea na vijana wanaondelea na mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara katika Kituo Atamizi cha Vijana cha Kilimobiashara (SUA-AIC Youth Agribusiness Incubators) mjini Morogoro

“Vijana tunatambua uwepo wenu hapa kituoni,jitahidini kujifunza mbinu bora za kilimo mkilenga kujiajili  na mwisho wa mafunzo yenu mrudi vijijini na mijini kuwa walimu kwa vijana wenzenu” alisema Kusaya

Katibu Mkuu Kusaya aliwapongeza vijana hao kwa kuamua kujiunga na kambi atamizi kwani wanatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli ya kuwataka vijana kujiajili kupitia kilimo.

“Lengo la serikali ya Awamu ya Tano ni kukifanya kilimo kuwa ni ajira na kazi inayochangia kukuza uchumi wa nchi,ndio maana nimekuja kuwatembelea na kuwatia moyo “ alisisitiza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo

Akitoa taarifa ya kituo hicho,Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof. Raphael Chibunda alisema kituo atamizi kinafundisha vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali wanaopenda kufanya kilimo biashara .

Alisema kwa sasa kuna vijana wapatao 40 wanaoendelea na mafunzo kwa vitendo kwa mwaka mmoja wakizalisha mazao ya mboga mboga kama hoho za rangi,matango na nyanya kwa usimamizi wa wataalam wa chuo.

Akielezea manufaa ya kituo hicho Hefsiba Olloo kutoka Kilimanjaro alisema ameweza kuzalisha nyanya kwenye kitalu nyumba na kuvuna kilo 1,318 za nyanya zilizompatia shilingi milioni 4 ndani ya kipindi cha miezi minne .

Mafanikio aliyopata  mwaka huu Januari alivuna kilo (338) Februari (400),Machi (400) na Aprili amevuna (180) ambazo ameuza kwa bei ya shilingi 2500 hadi 3000 kwa kilo moja .

 “ Kwa muda mfupi tangu nimejiunga na kambi atamizi hapa SUA mwezi Septemba 2019 tayari nimeona manufaa yake kwa kuwa na uhakika wa kipato kupitia kilimo cha nyanya .Nilipanda nyanya mwezi Octoba mwaka 2019 na sasa naendelea kuvuna” alisema Hefsida

Hefsida alihitimu shahada ya Sayansi  katika Hisabati (Bachelor of Science in Mathematics) Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2018 na hakuweza kupata ajira hivyo akaamua kuanzisha kilimo cha mboga

Kwa upande wake msimamizi wa kituo atamizi Zebedayo Sanga ambaye ni mhitimu wa digrii ya Horticulture mwaka 2018 toka SUA aliwahamasisha vijana wengi zaidi waliopo mitaani kuja kujifunza kilimobiashara na kuwa na uhakika wa kipato na ajira .
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com