Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Bariadi Mjini, Aprili 18, 2020 ambapo ameshiriki katika ibada ambayo waumini hao wameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli kwa Watanzania wote kuingia katika maombi ya siku tatu ( Aprili 17-19, 2020) kuliombea Taifa ili Mungu aliponye na janga la Corona.
Baadhi ya Wazee wa Kanisa wa Kanisa la SDA Bariadi mjini wakiwaongoza waumini wa kanisa hilo katika maombi maalum ya kuliombea Taifa, yaliyofanyika katika ibada Aprili 18, 2020 kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Watanzania wote kuingia katika maombi ya siku tatu ( Aprili 17-19, 2020) kuliombea Taifa ili Mungu aliponye na janga la Corona.(mwenye Tai wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka).
Baadhi ya waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Bariadi Mjini, Aprili 18, 2020 wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ambapo ameshiriki ibada ambayo waumini hao wameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Watanzania wote kuingia katika maombi ya siku tatu ( Aprili 17-19, 2020) kuliombea Taifa ili Mungu aliponye na janga la Corona.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa jumla ya watu 34 kati ya watu 120 waliokuwa kwenye uangalizi maalum (Karantini) mkoani Simiyu wameruhusiwa mara baada ya kupimwa na kukutwa hawana maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (COVID-19).
Mtaka ameyasema hayo Aprili 18, 2020 wakati akizungumza na waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Bariadi Mjini, ambao wameitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa Watanzania kuingia katika maombi ya siku tatu (Aprili 17-19, 2020) kuliombea Taifa ili Mungu aliponye na janga la Corona.
“Tulikuwa na watu 120 waliokuwa chini ya uangalizi ambao pia wamekuwa wakipata elimu kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona ili wakitoka wakawe msaada kwa familia zao; mpaka sasa watu 34 wameruhusiwa baada ya kupimwa na kuthibitika kwamba hawana maambukizi ya Corona, sisi kama mkoa tunaendelea kuchukua tahadhari zote,”alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa waliowekwa karantini ni pamoja na wanaofanya biashara nchi jirani ambao waliomba wenyewe ili wajitenge na familia zao; pia wapo baadhi ambao familia ziliomba Serikali iwaweke kutokana na kujua kuwa wametoka nchi zenye maambukizi kwa hofu ya kupeleka maambukizi kwa familia zao ikiwa itatokea wameambukizwa virusi vya Corona.
Aidha, Mtaka amesema kuwa mpaka sasa mkoa wa Simiyu hauna mtu mwenye maambukizi ya Virusi vya Corona na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari huku wakimuomba Mungu bila kukoma ili aliponye Taifa na janga la kidunia la ugonjwa wa COVID 19.
Katika hatua nyingine Mtaka amewahimiza wazazi kuwasimamia watoto wao na kuhakikisha wanajisomea wakiwa nyumbani huku akiwaasa kutunza chakula na kuepuka kuuza mazao pasipo na ulazima wa kufanya hivyo.
Mchungaji wa Kanisa la SDA Bariadi Mjini, Marco Mlingwa amesema Kanisa hilo limepokea maelekezo ya Serikali na linaungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuliombea Taifa Mungu aliponye na janga la Corona.
Kwa upande wao waumini wa Kanisa la SDA Bariadi Mjini wamemshukuru Mhe. Rais kuruhusu ibada kufanyika kwa kuzingatia maelekezo ya watalaam wa afya na kubainisha kuwa wataendelea kumuomba Mungu aliepushe Taifa na Corona wakiamini kuwa Mungu atasikia wakiomba kwa imani na kwa bidii.
“Tunamshukuru Mhe. Rais kuruhusu ibada kuendelea kufanyika huku tukichukua tahadhari, sisi Wakristo tunaamini watu tukiomba kwa bidii Mungu anasikia maombi, hivyo tukikutana na kuomba kwa bidii Mungu atasikia na kutuokoa na ugonjwa huu wa COVID 19,” alisema Paul Jidayi muumini SDA na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa.
“Sisi kama Wasabato tuna vipindi vyetu vya afya na kupitia vipindi hivyo tumeshajifunza na kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kanisani na majumbani; pia tunaungana na Rais kuliombea Taifa tukiamini kuwa Mungu atatusikia maana hata zamani, nchi ya Ninawi walipelekewa taarifa kuwa wataangamizwa lakini walipomlilia Mungu aliwasikia na hawakuangamia,” alisema Mariam Manyangu.
0 comments:
Post a Comment