Na Bashiri Salum, Wizara ya Kilimo-Morogoro
Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA wametakiwa kuanzisha maduka ya mbegu katika maeneo walipo wakulima ili kuwapunguzia gharama ya kuzifuta Morogoro mjini.
Akizungumza na watumishi leo alipotembelea taasisi hiyo Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya amesema ASA ni Taasisi pekee ya mbegu nchini hivyo inatakiwa kuwafika wakulima wote nchini.
Huduma ya mbegu bora inatakiwa na kilia mkulima hivyo ni lazima ASA wafikirie namna ya kushusha huduma zao chini kwa wakulima wadogo tofauti na ilivyo kwa sasa alibainisha Katibu Mkuu.
Akitolea mfano wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ambako ASA wanalo shamba kubwa la kuzalisha mbegu-(Msimba seed farm) Katibu Mkuu amesema wakulima wa maeneo hayo wanalazimika kwenda Morogoro mjini kununua mbegu
“Naagiza muanzishe maduka ya mbegu bora katika maeneo muhimu ili wakulima wapate mbegu bora zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao yao.Ningependa kuwepo na mahusiano mazuri kwenye
Halmashauri zinazowazunguka kwa kuweka maduka ya mbegu zenu iwe nafuu kwa wakulima wao kutozifuata mbali”.Alisema Katibu Mkuu.
Aidha ameipongeza taasisi hiyo kwa kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu bora na kutumia rasilimali zake za mashamba kuwapatia makampuni mengine ya mbegu ili uzalishaji wa mbegu uweze kuimarika.
Hata hivyo amewataka watumishi wa ASA kufanya kazi kwa ushirikiano na uadilifu ili kuongeza ufanisi katika kazi ambapo itawafanya kufikia malengo waliojiwekea.
Awali Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge amesema wamejipanga kuanzisha wakala watakaosaidia usambazaji wa mbegu nchi nzima ili wakulima wadogo waweze kufikiwa na mbegu hizo ambazo ni bei nafuu.
Hata hivyo Dkt Sophia amesema kiasi cha mbegu kinachozalishwa na ASA Pamoja na makampuni mengine ni tani elfu 59 ambazo kati ya hizo tani elifu 35 ni mbegu za pamba hivyo kiasi kilichobaki ni tani elfu 24 ambazo ni mazao mengine.
Amebainisha kwamba bado kama taifa kuna changamoto ya mbegu na kumuomba Katibu Mkuu ziangaliweji tihada nyingine za kuifanya sekta ya mbegu kuwa kivutio ili sekta binafsi ziweze kuendelea kuwekeza .
Hata hivyo watumishi wamemuomba Katibu Mkuu kusaidia vitendea kazi vikiwemo magari na maghala katika mashamba ya mbegu pamoja na ukarabati wa barabara za kuingia mashambani ili kuweza kuongeza uzalishaji wa mbegu bora.
0 comments:
Post a Comment