Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali bungeni jijini Dodoma, Februari 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza swali kutoka kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni Freeman Mbowe, bungeni jijini Dodoma, Februari 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano haiongozwi kibabe na kwamba hakuna mbunge yeyote wala diwani aliyezuiwa na Serikali kufanya shughuli zake kisiasa katika eneo lake.
“Nakanusha kwamba Serikali inaongozwa kibabe. Serikali haiongozwi kibabe na Mheshimiwa Mbowe sisi sote ni viongozi na kawaida huwa tunabadilishana mawazo kwa lengo la kulifanya Taifa liwe salama na Watanzania tunaowaongoza wapate maendeleo.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Februari 6, 2020) wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali ya papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Kiongozi huyo alitaka kujua ni lini Serikali itaruhusu vyama vifanye uenezi kuelekea uchaguzi mkuu, pia Serikali ina mpango gani kuwezesha kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi ili uwe huru na wa haki. Alisema ni wakati muafaka kwa wadau kukutana kuliko Serikali kutumia ubabe.
Waziri Mkuu amesema vyama vya siasa havijazuiwa kufanya shughuli zake, ila umewekwa utaratibu muhimu unaoviwezesha vifanye shughuli zake vizuri na kama kuna shida yoyote, wahusika wanatakiwa watoe taarifa.
“Mfano ni mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye alisema anazuiwa na OCD asifanye shughuli za siasa kwenye eneo lake, nilimuita hapa Bungeni, alikuja tukazunguza na suala hilo likaisha. Serikali inashirikiana na vyama vyote, kama kuna shida tuwasiliane.”
Kuhusu suala la vyama kuanza kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Waziri Mkuu amesema kwamba ratiba zitatolewa na zitaeleza ni lini kampeni zitaanza ili waweze kueleza sera zao na wananchi waendelee kufanya uamuzi wa sera ipi inafaa kuleta maendeleo nchini.
Kadhalika, kuhusu kuwa na tume huru ya uchaguzi, Waziri Mkuu amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni chombo huru na kimeundwa kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977, ibara ya 74 kipengele cha (7), (11) na (12) ambayo imeeleza kwamba chombo hicho ni huru na hakipaswi kuingiliwa na mamlaka yoyote.
Waziri Mkuu amesema suala la kuona Tume ya Taifa ya Uchaguzi si huru ni mtizamo wa mtu binafsi lakini ni chombo huru kama Katiba inavyoonesha. “Hatujawahi kuona chombo hiki kikiingiliwa hata na Rais, kama kuna tatizo semeni lifanyiwe kazi.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa atoe taarifa ya hatua iliyofikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhusu mapitio ya gharama za huduma ya maji nchini.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Mjini, Mheshimiwa Pauline Gekul aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa mapitio ya gharama za huduma ya maji.
“Serikali hailengi kufanya biashara wala kupata faida; muhimu ni wananchi wapate huduma. Tumeunda kamati na mamlaka za utoaji huduma za maji kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusimamia ujenzi na uendeshaji wa miradi ya maji.”
0 comments:
Post a Comment