METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, February 21, 2020

RC ALLY HAPI, KULIPA KODI NI FAHARI NA UZALENDO

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Ally Hapi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wanafanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo baada ya kumsalimia ofisini kwake na kumtaarifu maendeleo ya kampeni
hiyo.
Afisa Msimamizi wa Kodi Bw. Chama Siriwa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akimuelimisha mfanyabiashara wa duka la dawa muhimu wa Manispaa ya Iringa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika
mkoani humo.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakikagua Cheti cha Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) cha mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi wa Manispaa ya Iringa kabla ya kumpatia elimu ya kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea kufanyika mkoani
humo

Wito umetolewa kwa wafanyabiashara wote nchini kulipa kodi kwa wakati na hiari ili kusaidia maendeleo ya nchi kwa sababu kulipa kodi ni jambo la fahari na uzalendo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Ally Hapi wakati alipotembelewa na timu ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wapo mkoani humo wakifanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi.

“Wito wangu kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Iringa na maeneo mengine ni kwamba kila mfanyabiashara afahamu kuwa, kulipa kodi ni jambo la fahari na uzalendo hivyo ni wajibu wa kila mfanyabishara kuhakikisha analipa kodi kwa wakati ili kusaidia maendeleo ya nchi yetu na
sekta mbalimbali ambazo zinategemea kodi katika kujiendesha”, alisema Mhe. Hapi.

Mkuu wa Mkoa huyo pia amewahimiza wafanyabishara kutembelea Ofisi za TRA zilizo karibu na maeneo yao kwa ajili ya kupata uelewa na ushauri wa masuala mbalimbali ya kikodi ambayo yatawasaidia wasifanye makosa.

“Mamlaka yetu sasa imepanua huduma zake zaidi, kwa wale wafanyabishara ambao wanatatizwa na masuala ya kikodi, nitumie fursa hii kutoa wito kwao kwamba, tunazo Ofisi za Mamlaka ya Mapato katika wilaya zetu zote, waweze kufika kwa ajili ya kuuliza, kupata uelewa na pengine kupata ushauri ambao utawasaidia wasiingie katika makosa ya kikodi.

“Tunatamani kuwa na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao vizuri lakini pia pale wanapopata mkwamo wa aina yoyote wasisite kuwasiliana na Mamlaka ya Mapato katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa wanapata ushauri sahihi”, Alieleza Mhe. Hapi.

Mhe. Hapi aliongeza kuwa kila mfanyabiashara ana mchango katika maendeleo yanayopatikana ndani ya Taifa hili, hivyo ni muhimu watu wawe na utamaduni wa kulipa kodi ili Serikali iweze kutekeleza majukumu yake na wao wawe na haki ya kudai na kuona fahari juu ya maendeleo
yanayofanyika nchini.

Awali, kiongozi wa timu ya maafisa wa TRA wanaofanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo Bi. Rose Mahendeka, alimueleza Mkuu wa Mkoa huo kuwa, tayari timu hiyo imeshawafikia wafanyabiashara takribani 600 katika Wilaya ya Kilolo na inaendelea na kampeni katika Wilaya ya
Iringa mjini na Mufindi.

Timu ya elimu kwa mlipakodi inapita mlango kwa mlango katika maduka ya wafanyabiashara ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara wanaelimishwa juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kodi na wanakumbushwa kulipa kodi kwa hiari na wakati.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com