METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, January 7, 2020

WAZIRI HASUNGA AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI NJOMBE, ATOA MAAGIZO MAZITO KWA TOSCI, TFRA NA TPRI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa maghala na Vihenge vya Kisasa (Silos) wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA kanda ya Makambako wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe, tarehe 7 Januari 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua mradi wa Umwagiliaji wa Itipingi  uliopo Wilayani Njombe wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe, tarehe 7 Januari 2020. 
 Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua akikagua hali ya upatikanaji wa mbolea kwenye ghala la kampuni ya ETG Katika Halmashauri ya Mji mdogo wa Makambako wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe, tarehe 7 Januari 2020. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua ujenzi wa maghala na Vihenge vya Kisasa (Silos) wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA kanda ya Makambako wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe, tarehe 7 Januari 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo kuhusu umuhimu wa miradi ya umwagiliaji nchini mbele ya wakulima mara baada ya kukagua mradi wa Umwagiliaji wa Itipingi  uliopo Wilayani Njombe wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe, tarehe 7 Januari 2020. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Njombe

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameitaka Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha kuwa inasimamia utekelezaji wa maagizo ya serikali ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanauza mbolea kwa bei elekezi ili kuwanufaisha wakulima kwani mbolea ni miongoni mwa Pembejeo muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wakulima wanalima mazao yenye tija.

Alisema kuwa mfanyabiashara yeyote atakayebainika kuuza mbolea zaidi ya bei elekezi anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni ya kufanya biashara hiyo.

Waziri Hasunga ametoa agizo hilo tarehe 7 Januari 2020 wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Njombe ambapo amekagua hali ya upatikanaji wa mbolea kwa kukagua maghala ya kuhifadhia mbolea na kuiagiza TFRA ndani ya siku saba kuhakikisha kuwa mbolea ya kukuzia UREA inapatikana mkoani hapa.

Kuhusu Mbegu za mazao, Mhe Hasunga ameitaka Taasisi ya Udhibiti wa mbegu nchini (TOSCI) kuhakikisha kuwa mbegu zinazopelekwa kwa wakulima nchini zinakuwa katika ubora unaostahili huku akiagiza wauzaji wa mbegu feki kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima nchini kuhusu uwepo wa mbegu feki hivyo naiagiza TOSCI kuhakikisha inakomesha mbegu hizo ili wakulima waweze kunufaika na uzalishaji wa mazao yao” Alikaririwa Mhe Hasunga

Kwa upande wa Viuatilifu, Waziri Hasunga ameiagiza Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu ukanda wa Kitropiki (TPRI) kuhakikisha wanafanya ukaguzi nchi nzima ili kubaini na kuondoa viuatilifu feki vyote sokoni ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwanyang’anya leseni wafanyabiashara wanaofanya biashara hiyo kinyume na maelekezo ya serikali.

Ameongeza kuwa TFRA inapaswa kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima kote nchini kuhusu matumizi sahihi ya Viuatilifu ili kuondoa dhana ya wakulima kuwa na malalamiko mengi kuhusu viuatilifu.

Aidha, Mhe Hasunga amesisitiza kuwa serikali inayoongozwa na Dkt Magufuli haitawapangia bei ya mazao yao wakulima hususani mazao makuu ya chakula na biashara kwani wakulima wanapokuwa wanalima mazao yao hakuna watu wanaowasaidia hivyo wakati wa kuuza pia wanapaswa kuamua bei kulingana na soko.

Mhe Hasunga pia amepongeza maendeleo ya ujenzi wa mradi maghala na vihenge vya kisasa unaofanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA kanda ya Makambako ambapo amesema kuwa wakandarasi wote wanapaswa kukamilisha ujenzi haraka iwezekanavyo kwani serikali haitoongeza muda kwa wakandarasi hao watakaoshindwa kukamilisha majukumu yao ndani ya muda wa mradi.

Katika hatua nyingine Mhe Hasunga ameipongeza Tume ya Umwagiliaji nchini kwa kusimamia na kuwa na ukamilifu wa mradi wa Umwagiliaji wa Itipingi wa kikundi cha Twilumba kilichopo Wilayani Njombe uliojengwa kwa jumla ya Tsh Milioni 400 wenye urefu wa mita 1725 uliojenga Mfereji pamoja na Banio.

Kuhusu changamoto za masoko ya mazao yao, Waziri Hasunga awahakikishia kuwa serikali imeanzisha kitengo cha masoko cha wizara ya Kilimo hivyo wakulima wa mazao yote hawapaswi kuwa na mashaka na soko la mazao yao.

MWISHO 
Share:

1 comment:

  1. Tunaipokea kwa mikono miwili kauli hiyo Kama wauzaji na watoa huduma za pembejeo

    ReplyDelete

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com