Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama, wakati akiwasili, katika ukumbi wa Hazina
jijini Dodoma, Juni 15.2019, kwenye Kongamano la Nne la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi, katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’I Issa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua
taarifa ya utekelezaji wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, kwenye Kongamano
la Nne la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, lililofanyika katika ukumbi wa
Hazina jijini Dodoma, Juni 15.2019, kutoka kushoto ni Katibu Mtendaji wa
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’ Issa,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu,
Jenista Mhagama, Mwenyekiti wa Baraza hilo Dk. Festus Limbu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akihutubia
wananchi na baadhi ya viongozi wa serikali, kwenye Kongamano la Nne la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, lililofanyika katika ukumbi wa Hazina
jijini Dodoma, Juni 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
……………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa mwaka
mmoja kwa viongozi wa mikoa ya Dar-es-salaam, Morogoro, Iringa, Njombe,
Mbeya, Rukwa, Singida na Shinyanga ihakikishe iwe imekamilisha kuandaa
Mwongozo wa Uwekezaji.
Pia amewataka viongozi wa mikoa na
halmashauri zote nchini wahakikishe wanaanzisha vituo vya uwezeshaji
wananchi kiuchumi kama kile cha Kahama ili kuharakisha nia ya Serikali
katika kuwezesha wananchi kiuchumi.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Juni
15, 2019) wakati akifungua Kongamano la Nne la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. Kongamano hilo
limeandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi(NEEC) na
kauli mbiu yake ni Wezesha Watanzania Kujenga Viwanda.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuratibu
mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo ya Serikali na ile
ya binafsi ili kujua ipo mingapi na inamnufaisha nani na je wanufaika
wanajijua na ni kweli wananufaika na kisha wampelekee taarifa.
Waziri Mkuu amesema mikoa yote
iliyokamilisha kuandaa mwongozo wa uwekezaji, nayo ifikapo mwakani
inapaswa kuonesha hatua za utekelezaji katika kutumia fursa mbalimbali
zilizoainishwa pamoja na mikakati ya kutangaza fursa hizo zilizopo
katika maeneo yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema matokeo ya
tafiti ziliyofanywa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
kuhusu biashara na uwekezaji nchini yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi
kikubwa katika uandaaji wa maandiko ya miradi mikubwa inayopendekezwa na
shirika hilo.
“Miradi hiyo ni pamoja na ule wa
“Harmonized Innovation Solutions for Local Economic Development” ambao
upo katika hatua za maandalizi. Lengo la UNDP ni kuhakikisha kuwa miradi
inayohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi inatekelezwa moja kwa moja na
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo lipo chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.”
Amesema NEEC ina uwezo mkubwa katika
kusimamia miradi mbalimbali ya uwezeshaji ambayo imekuwa ikifadhiliwa na
Serikali pamoja na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo UNDP, ILO, UNCTAD, AfDB
na UN-Women, hivyo ameyahakikishia mashirika hayo kuwa
Serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yote ili kupata
matokeo yaliyo tarajiwa.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuziagizamamlaka zote zishirikiane na NEEC kuhakikisha kuwa fursa za
uwezeshaji wananchi kiuchumi zilizobainishwa kupitia tafiti za UNDP
zinafanyiwa kazi. “Aidha, hakikisheni kuwa Miradi mikubwa ya uwezeshaji
wananchi kiuchumi inatokana na tafiti hizo”
Amesema anaimani kubwa kuwa kupitia
utekelezaji wa miradi hiyo, malengo mbalimbali ya nchi kuhusu uwezeshaji
wananchi kiuchumi yatafikiwa. Baadhi ya malengo hayo ni pamoja na
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020; Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano; Dira ya Taifa ya Miaka 25; na Malengo Endelevu ya
Maendeleo ya umoja wa Mataifa (SDGs).
Pia Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Taifa
la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi liendeleekuratibu masuala ya uwezeshaji
wananchi kiuchumi ikiwemo utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha
2015 – 2020 kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa
vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.
“Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
iboreshwe sambamba na kuongeza ufanisi ili iweze kuwafikia Watanzania
wengi hususan wale wa vijijini. Vilevile, kamilisheni na hakikisheni
mnazindua haraka mfumo wa kupima mifuko ya uwezeshaji kwa matokeo ya
kiuchumi na kijamii na siyo kwa shughuli walizofanya.”
Amesema uwezeshaji wananchi kiuchumi ni
suala mtambuka, sekta mbalimbali za kiuchumi na sekta binafsi
zinajihusisha moja kwa moja katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hivyo,
amesisitiza kwamba ni muhimu sana masuala ya uratibu, ufuatiliaji na
tathimini ya shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, yakafanywa mara
kwa mara ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
0 comments:
Post a Comment