Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akiwasilisha
azimio la kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki mbele ya Bunge hii
leo mjini Dodoma. Bunge limeridhia Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki na
Serikali imeandaa Mpango kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki
kwa wachimbaji wadogo ambao umeainisha fursa mbalimbali.
………………………
Na Lulu Mussa
Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene amesema
inakadiriwa kuwa asilimia 25 hadi 33 ya wachimbaji wadogo wa dhahabu
hapa nchini, wameathiriwa na Zebaki kwa kupata magonjwa yakiwemo yale ya
mifumo ya neva za fahamu, uzazi, upumuaji, figo, moyo, na udhaifu wa
mwili.
Akiwasilisha azimio la Bunge
la kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu zebaki Simbachawene amesema,
baadhi ya athari kwa mazingira zilizobainika kutokana na matumizi ya
zebaki ni pamoja na kudhoofika kwa ukuaji wa viumbe hai wanaoishi ndani
ya maji; uchafuzi wa mfumo mfuatano wa mazao ya chakula, mifugo na
samaki; na uchafuzi wa vyanzo vya maji, hewa na udongo.
“Lengo kuu la Mkataba huu ni
kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari za uchafuzi wa
mazingira unaotokana na matumizi ya Zebaki katika hatua za uzalishaji,
matumizi na utupaji wake” Simbachawene alisisitiza.
Simbachawene ameainisha sheria
ambazo zinatoa mwongozo wa jumla kuhusu usimamizi wa Zebaki ikiwa ni
pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004); Sheria ya Udhibiti na
Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani (2003); Sheria ya
Madini (2010); Sheria ya Afya ya Jamii (2009); Sheria ya Usalama na Afya
Mahali pa Kazi (2003); na Sheria ya Chakula na Dawa (2003) na
kusisitiza kuwa zitaandaliwa kanuni za Usimamizi wa Zebaki chini ya
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004) ili kuwezesha utekelezaji wa
Mkataba huu.
Tafiti zinaonyesha kuwa zebaki
hudumu katika mazingira kwa muda mrefu (miaka 2 hadi 20) na husafiri
masafa marefu kwa njia ya hewa, maji (mito, maziwa na bahari) na udongo
umbali hadi kilomita 1,000 kutoka kwenye chanzo; na kuathiri afya ya
binadamu, viumbe wengine na mazingira. Athari hizi zinajitokeza zaidi
katika nchi zinazoendelea ukilinganisha na nchi zilizoendelea kutokana
na nchi hizo kupunguza matumizi ya Zebaki.
Awali akiwasilisha hoja za
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mwenyekiti
wa Kamati hiyo Mhe. Suleiman Ahmed Sadiq amesema Kamati ianona umuhimu
wa nchi kuridhia Mkataba huu kwa lengo la kushirikiana na nchi nyingine
kutafuta suluhisho la zebaki bila kuathiri shughuli za wachimbaji
wadogo.
“Ushauri wa Kamati ni kuwa
Serikali ijitahidi kuhakikisha inapatikana teknolojia rahisi na rafiki
kwa wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu” alisisitiza Mhe. Sadiq.
Zebaki ni miongoni mwa
kemikali zinazohatarisha zaidi afya ya jamii duniani kutokana na kudumu
katika mazingira kwa muda mrefu, kusafiri masafa marefu kwa njia ya
hewa, maji (mito, maziwa na bahari) na udongo na hivyo kuathiri afya ya
binadamu na mazingira. Jumla ya nchi 113 zimeridhia Mkataba huu ambao
ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 16 Agosti, 2017 mara baada ya Nchi 50
kuridhia kama inavyotakiwa na Ibara ya 30 ya Mkataba wa Minamata.
0 comments:
Post a Comment