NAIBU Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema
misingi ya utafiti ni jambo muhimu na la msingi litakalopaswa
kuzingatiwa katika uchapishaji na utangazaji wa taarifa mbalimbali ili
kuweza kulinda misingi ya amani iliyopo nchini.
Akizungumza
leo Jumanne (Julai 9, 2019) Jijini Dar es Salaam katika Kongamano maalum
la siku ya Amani lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TANTRADE) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar
es Salaam (DITF), Dkt. Tulia alisema uchapishaji na utangazaji wa
taarifa yoyote haina budi kuwa na tija katika taifa.
Dkt. Tulia
alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na utamaduni uliozoeleka
wa kutangaza na kuchapisha taarifa mbalimbali katika jamii kupitia
vyombo vya habari pasipo na kuzingatiwa kwa misingi ya utafiti hatua
inayoweza kuleta migongano isiyo na tija kwa taifa.
“Serikali ya
Awamu ya Tano tunaona inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo
mradi wa umeme katika Mto Rufiji, sni wajibu wetu kulinda misingi ya
amani iliyopo ili tuone matunda ya miradi hii katika nchi yetu” alisema
Tulia.
Aidha Dkt.
Tulia alisema ni wajibu wa misingi ya utafiti ikazingtiwa katika taaluma
mbalimbali ikiwemo ya uandishi wa habari kwani wapo baadhi ya watu
wanaofikiri kuwa wanaweza kuandika na kutangaza habari pasipo na kusomea
taaluma hiyo, jambo ambalo si la kweli kwa kuwa uandishi wa habari ni
taaluma nyeti na muhimu kama zilivyo taaluma nyingine.
Aliongeza
kuwa ni wajibu wa Watanzania wote kusoma vitabu mbalimbali
vilivyoandikwa na waasisi wa taifa vikiwemo vitabu vya Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambavyo vimekuwa na wingi wa maarifa na
maelekezo yanayopaswa kuzingatiwa ili kuweza kujenga taifa lenye umoja,
upendo na mshikamano.
Naye Mkuu wa
Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano Zanzibar, Imane Duwe alisema
mfumo wa soko huria nchini yameleta mabadiliko makubwa katika tansia ya
habari na mawasiliano ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii, ambayo
imekuwa imeleta hamasa kubwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo
vijana.
“Hapo awali
mwandishi wa habari alipokuwa akitumwa kazi na mhariri wake ni lazima
arudi na atoe taarifa kwa mkuu wake pamoja na habari au taarifa hiyo
kuweza kufanyiwa uhariri kabla ya kuchapishwa na kutangazwa lakini kwa
sasa hali ni tofauti kidogo, kwani tukio lolote linaweza kutumwa wakati
huo huo kupitia vyombo vya kisasa zaidi vya mawasiliano” alisema.
Aliongeza
kuwa vyombo vya habari vya zamani ikiwemo Magazeti, Redio na Televisheni
kwa sasa navyo vimeingia katika ushindani mkubwa wa soko kwani kwa
upande wao pia wameanzisha mitandao mbalimbali ya kijamii ili kuweza
kuwa na njia za kisasa zaidi za mawasiliano.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema ni
wajibu wa Viongozi na Watanzania wajenge utamaduni wa kuheshimu tunu na
misingi mikuu ya amani nchini ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, misingi ya Azimio la Arusha ambayo iliasisiwa na Hayati Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha
aliongeza kuwa ili kuweza kujenga Taifa lenye misingi bora ya amani ni
wajibu wa Serikali kupitia Viongozi kuwa na matumizi na usimamizi bora
wa rasilimali za taifa na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wote
pamoja na kuweka misingi imara katika ulinzi rasilimali hizo.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Baraza la Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa
Salum alisema Tanzania inaweza kufikia na kufanya mapinduzi makubwa
katika sekta ya viwanda iwapo Viongozi wataweka mkazo katika usimamizi
wa rasilimali watu yenye kutambua umuhimu wa kulinda amani, weledi,
uzalendo na kujiamini.
“Moja ya
Nguzo muhimu katika kufikia uchumi wa viwanda ni mfanyakazi, hivyo ni
wajibu kila mwenye dhamana hiyo kutimiza wajibu wake huku akiogopa
kufanya vitendo vya ufisadi kwani hata katika vitabu takatifu
vimezungumzia ufisadi ni jambo baya sana” alisema Sheikh Salum.
0 comments:
Post a Comment