METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 19, 2019

MAKAMU WA PILI WA RAIS AFUNGUA TAMASHA 24 LA UTAMADUNI WA MZANZIBARI

Na Mwashungi Tahir,Maelezo

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi  aliwataka vijana kuacha kuvutika na desturi za kigeni kwa kuacha mila zao  kwani kunaweza kusababishia ukiukwaji wa maadili  kwa Taifa la Wazanzibar.

Wito huo aliutoa huko  katika Uwanja wa Kumbu Kumbuwa Mapinduzi Square  wakati alipokuwa akifungua Tamasha  la 24 la Utamaduni wa Mzanzibar na kuwataka vijana  waendeleze silka , tamaduni  na mila za Kizanzibar ili jamii isipotee.

Alisema Vijana hawafuati mfumo  halisi wa maisha uliowakuza na hatimaye wamekuwa wahanga wa kuiga, kukumbatia na kufuata  tamaduni ambazo kimfumo haziendani na mazingira  pamoja   na mfumo mzima wa maisha ya Wazanzibar.

Hivyo alisema wakati umewadia kuacha utamaduni wa kigeni na kila siku tujivunie mambo ya Wazanzibar na kuwa na mikakati mbali mbali itayosaidia kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuenzi kulinda na kuendeleza utamaduni  wa Zanzibar.

Pia alieleza kwamba tukiendelea kuadhimisha tamasha hili jamii ina wajibu wa kujiuliza na kupata jibu la pamoja kwa kiasi kipi matamasha haya yananandaliwa katika visiwa vya Unguja na Pemba na kuweza kubeba dhima na kusaidia ukuzaji na uendelezaji  wa mfumo wa utamaduni na sanaa  katika jamii ya Zanzibar.

Vile vile alikemea matendo maovu ambayo yanakosa uadilifu na kusababisha kuzaa chuki , mifarakano, visasi baina ya familia na kuhatarisha mshikamano wa kijamii ambao husababisha uvunjifu na amani, kutia aibu Taifa na watu wake .

Aliiomba jamii kuiunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika vitendo vua udhalilishaji kwa kuacha muhali au kuoneana haya jamii ijitokeze kutoa ushahidi katika vyombo vya sheria hatimae sheria ichukuwe mkondo wake tukishirikiana kwa pamoja tunaweza na kuondosha madawa ya kulevya ili tupate vijana walio bora katika nguvu kazi.

“naomba vijana wajiepushe na madawa ya kulevya ili Taifa lipate vijana walio imara na kupatikana Taifa lililo bora”,alisema Balozi Seif.

Nae Waziri wa Vijana , Utamaduni, Sanaa na Michezo Ali Abeid Karume alisema Tamasha la Mzanzibar tutalienzi kwa lengo la kukuza mila silka na utamaduni ili jamii waweze kujua mambo ya visiwa hivi na kizazi  kiendelee kujua mambo ya nchi yao yakiwemo mambo ya asili .

Alisema tamasha hili mwaka ujao linatimiza miaka 25 ambalo litakuwa linaingia robo karne hivyo amewataka wananchi kutarajia  tamasha kuwa kubwa zaidi .

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud alitoa rai kwa Wizara ya Vijana , Utamaduni , Sanaa na Michezo kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ianze mitaala ili watoto waanze wakiwa wadogo kufundishwa mambo ya utamaduni ili usipoitee.

Alisema dhamira kubwa ya tamasha hili ni kutunza utamaduni , utu mila na silka za kizanzibar .

Kauli mbiu ya tamasha hili ni”Utamaduni ni Ngao na ustawi wa jamii yetu” .

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com