Meneja wa Wakala wa Vipimo Tabora akitoa
elimu ya matumizi sahihi ya mizani kwa Wakulima wa kijiji cha Mtunguru
waliokuja kuuza pamba zao katika Chama cha msingi cha ushirika cha
Nguzujise
Afisa Vipimo Mkoa wa Tabora akihakiki
usahihi wa mizani inayotumika kununulia pamba kwa kutumia jiwe maalumu
la Wakala wa Vipimo.
Afisa Vipimo Mkoa wa Tabora akihakiki usahihi wa mizani inayotumika kununulia pamba kwa kutumia jiwe maalumu la Wakala wa Vipimo
Wananchi wakioneshwa alama za kukagua ili kubaini usahihi wa mizani kabla ya kuuza pamba
Stika ya Wakala wa Vipimo ikiwa imebandikwa katika mizani iliyohakikiwa
Pamba ikiwa tayari kwa ajili ya upimaji
……………………..
Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Tabora
inaendelea kufanya uhakiki wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika
pamoja na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo katika Wilaya
mbalimbali za mkoa wa Tabora ili kuweza kuwalinda wakulima wa zao la
pamba waweze kupata faida kwa kuuza mazao yao (pamba) kwakutumia vipimo
mizani sahihi iliyohakikiwa na wakala wa Vipimo.
Meneja wa WMA Tabora ndugu Mrisho
Mandari, amesema kuwa mpaka sasa Wakala wa Vipimo Tabora imeshafanya
uhakiki wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya tano za
Mkoa wa Tabora ambazo ni Igunga, Nzega, Uyui, Urambo pamoja na Kaliua.
Katika wilaya zote Jumla ya Mizani 158 imehakikiwa na Wakala wa Vipimo
na kusambazwa katika vituo vyote vya kununulia pamba Mkoani hapo.
Amesema kuwa, Kati ya Mizani 158
iliyohakikiwa jumla ya mizani 130 ilipitishwa haikubainika kuwa na
tatizo lolote, na mizani 18 ilikutwa na hitilafu ndogo ndogo ambapo
baadaye zilirekebishwa na 16 kati ya hizo zilifikia wigo wa usahihi.
Mizani miwili ilikataliwa kabisa kutumika kutokana na matatizo yake kuwa
makubwa.
Ndugu Mrisho Mandari, amesema kuwa mara
baada ya kukamilisha uhakiki wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika
(AMCOS), sasa wanatoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa Wakulima wa
pamba na wanachi wote kwa ujumla ili waweze kutambua mambo muhimu ya
kuzingatia mara wanapoenda kuuza pamba katika vituo maalumu
vilivyoandaliwa.
Pia, amewaasa wakulima wawe makini pindi
wanapoenda kuuza pamba kwa kuhakikisha mizani inasoma sufuri (0) kabla
ya kuanza upimaji kwa kutumia mizani ya digitali. Mara baada ya kupima
furushi la pamba mizani inatakiwa kurudi katika sufuri, na wahakikishe
mizani haisomi hasi (-) baada ya kutoa mzigo na ikitokea imesoma hasi
mwambie karani anayesimamia mizani aweze kuizima na kuiwasha tena
mizani hiyo kisha zoezi la upimaji liendelee.
Wakala wa vipimo inaendelea kuboresha
ulinzi katika mizani zinazotumika katika ununuzi wa zao la pamba, kwa
mizani iliyohakikiwa na kukudhi vigezo inawekewa stika maalumu ya Wakala
wa Vipimo pamoja na kufunga lakiri katika maeneo muhimu ya mizani ili
kuzuia mizani isije ikachakachuliwa na wanunuzi wa pamba wasio
waaminifu.
Vilevile, amewataka wanunuzi wa pamba
waweze kujiepusha na viendo vya dhuruma kwa wakulima wa pamba kwa
kutumia mizani ambazo hazija hakikiwa na kupata idhini ya kutumika
katika msimu wa ununuzi wa pamba. Amewakumbusha kuwa kwa sasa sheria ya
vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002 imefanyiwa marekebisho
na adhabu zimekuwa kali ambapo ukikutwa na kosa la kuchezea mizani na
ukakiri faini yake ni kiasi kisichozidi shilingi milioni ishirini
(20,000,000/=) kwa kosa la kwanza na kiasi kisichozidi milioni hamsini
(50,000,000/=) kwa mkosaji wa kosa la kujirudia.
Zoezi hili la uhakiki wa mizani na utoaji
elimu kwa wakulima wa pamba ni zoezi endelevu ambalo hufanyika mara kwa
mara ili kuwalinda wakulima wa pamba na hufanyika kabla ya kuanza kwa
msimu wa ununuzi wa pamba na mara baada ya kuanza kwa msimu maafisa
vipimo hupita katika vituo mbalimbali vinavyotumika kununulia pamba na
kujiridhisha kama mizani inatumika kwa usahihi bila kupunja kama ilivyo
hakikiwa.
Wakala wa vipimo inatoa wito kwa
Wafanyabiashara na Wakulima wote kuhakikisha wanazingatia matumizi ya
vipimo sahihi na kujiepusha na uchezeaji wa vipimo na endapo mkulima
utakutana na udanganyifu wa aina yeyote atoe taarifa katika ofisi zetu
za wakala wa vipimo zilizopo makao makuu ya mikoa yote Tanzania Bara au
kupitia namba yetu ya bure kabisa ambayo ni 0800 11 00 97.
0 comments:
Post a Comment