Na Mwandishi Wetu.
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba SC wamekabidhiwa Kombe lao
baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Mtibwa Sugar katika mchezo wa mwisho wa
ligi hiyo jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems imemaliza
Ligi Kuu na pointi 93, zikiwa ni saba zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga
SC waliomaliza na pointi 86 katika nafasi ya pili, wakati Azam FC
imeshika nafasi ya tatu kwa pointi zake 75.
Hilo linkuwa taji la pili mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba SC
na la 20 jumla kihistoria baada ya awali kulibeba katika miaka ya 1965,
1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001,
2003, 2004, 2007, 2010, 2012 na 2018.
Watani wao, Yanga SC ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi Kuu, mara
27 wakiwa wamebeba taji hilo miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972,
1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998,
2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.
Timu nyingine zilizowahi kubeba taji hilo ni Cosmopolitan 1967, Mseto SC
ya Morogoro 1975, Pan African 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal
Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar mara mbili 1999 na 2000 na Azam FC
2014.
Wakati Simba SC ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo,
Stand United imeungana na African Lyon kuteremka daraja baada ya
kufungwa 2-0 na JKT Tanzania.
Nazo Kagera Sugar ya Bukoba na Mwadui FC ya Shinyanga zitamenyana na
timu za Daraja la Kwanza, Pamba SC na geita Gold kuwania kubaki Ligi Kuu
katika mechi za mchujo.
MATOKEO YA MECHI ZOTE ZA LIGI KUU LEO
Coastal Union 0-0 Singida United.
Mbeya City 0-0 Biashara United.
Mtibwa Sugar 0-0 Simba SC.
Ruvu Shooting 1-0 Alliance FC (Fully Zullu Maganga 25’ p) . .
JKT Tanzania 2-0 Stand United (Samweli Kamuntu 51’, Najimu Maguli 73’).
Ndanda SC 1-3 Mwadui FC (Kigi Makasi : Ottu Joseph 39’, 41’, Salim Aiyee 61’) .
Yanga SC 0-2 Azam FC (Daniel Amoah 45’+2, Mudathir Yahya 50’).
Mbao FC 1-1 Kagera Sugar (Hebert Lukindo 60’ : Ally Ramadhan 20’).
Tanzania Prisons 3-1 Lipuli FC (Benjamini Asukile 29’, Adam Adam 48’, 85’ : Seif Rashid 46’).
African Lyon 0-2 KMC FC (Cliff Buyoya 21’, 17’)
0 comments:
Post a Comment