METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, May 31, 2019

SERIKALI KUJA NA MBINU ZA ZIADA KUKABILIANA NA UGONJWA WA MNYAUKO WA MIGOMBA-MHE BASHUNGWA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 31 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo) 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kulia) pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) wakifuatilia kipindi cha maswali na majibu bungeni leo tarehe 31 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Kwa kipindi cha Mwaka 2006 - 2014, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Kagera umetoa mafunzo ya kutokomeza ugonjwa wa mnyauko wa migomba kwa wakulima na maafisa ugani kwenye wilaya zote zilizoathirika.

Serikali imekuwa ikiendesha kampeni ya kung’oa migomba yote iliyoathirika, kukata Ua Dume na kuiteketeza. Halmashauri zote za Wilaya za Mkoa wa Kagera ziliweka sheria ndogo ndogo za kuwataka wakulima kung’oa na kuchoma au kuzika migomba yote iliyoathirika. Zoezi hilo lilipunguza ueneaji wa ugonjwa huo kwa asilimia 70.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 31 Mei 2019 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe Jasson Samson Rweikiza Mbunge wa Bukoba vijijini aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani kuchukua hatua za makusudi za kupambana na ugonjwa huo na kutokomeza kabisa.

Bashungwa alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya tafiti za kuzalisha miche bora ambayo haina vimelea vya ugonjwa wa unyanjano kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ikishirikiana na Shirika la Belgium Technical Cooperation.

Aidha, hadi sasa miche bora milioni sita (6) imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Kagera na Kigoma.

Bashunwa ametoa wito kwa wakulima kote nchini kutumia mbegu bora za migomba aina ya Shia 17, Shia 23, Nshakara, Nyoya, na Kinohasha zinazozalishwa katika taasisi za utafiti kama Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine, Mikocheni, Uyole, Kibaha, Maruku na Tengeru ili kuongeza tija katika uzalishaji na kutosafirisha ndizi zilizofungashwa na majani ya migomba kutoka mashamba yaliyoathirika.

Aliutaja ugonjwa huo wa Mnyauko wa migomba ambao kitaalamu unaitwa unyanjano wa migomba kuwa husababishwa na vimelea aina ya bacteria ambao hushambulia aina zote za migomba na jamii yake.

Ugonjwa huo husambazwa na ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili; miche iliyoathirika; vifaa vya shambani vilivyotumika kwenye migomba iliyoathirika na vifungashio vya kusafirishia ndizi.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com