METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 9, 2019

WAZIRI MKUU: WAKANDARASI WA MAJI WALIPWA 138bn/-


 Asema sh. bilioni 44 zinaandaliwa kuwalipa wengine

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi sasa, Serikali imeshahakiki madai ya wakandarasi waliotekeleza miradi ya maji nchini na imewalipa shilingi bilioni 138.

“Hivi karibuni tutalipa fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 44. Ninaielekeza Wizara husika ihakikishe kuwa watendaji wa Serikali wanafuatilia ufanisi wa wakandarasi na wajiridhishe kuwa wakati wote unakuwa wa kiwango cha kuridhisha,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.

Alisema wakati wa michango yao, Waheshimiwa Wabunge walizungumzia upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na baadhi yao walikosoa utekelezaji na ubora duni wa baadhi ya miradi ya maji. Alisema wengine walionesha kutoridhishwa na utekelezaji huo kwani baadhi ya maeneo hayajafikiwa na miradi hiyo.

Waziri Mkuu alisema licha ya changamoto hizo, Serikali inaendelea na usambazaji wa maji, na itachukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inayotekelezwa, inatoa matokeo yaliyokusudiwa.

“Kwa kuanzia, Mheshimiwa Rais aliunda tume maalum ili kupitia, kufanya tathmini na kutoa mapendekezo juu ya hatua za haraka zinazostahili kuchukuliwa, kwa lengo la kuhakikisha thamani ya fedha kwa miradi hiyo inapatikana na kuleta tija,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema changamoto nyingine katika eneo la maji ni uharibifu wa mazingira ambao umeshika kasi kubwa na kwamba hatua za haraka hazina budi kuchukuliwa ili kuiepusha nchi na janga la ukame.

“Katika kuhakikisha kuwa tunaondokana na janga hili, Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 yenye lengo la kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira nchini.”

Alisema sheria hiyo pia itaongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma ya maji; kuleta uendelevu kwa miradi ya maji vijijini; kuimarisha ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji baada ya kuundwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

“Nawaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji, wachukue hatua za makusudi katika kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji na kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira. Viongozi na watendaji watakaobainika kutosimamia ipasavyo sheria husika, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge muunge mkono jitihada hizi za Serikali,” alisisitiza.

Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/- kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo sh. 116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com