Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Kambi za
Kitaaluma mkoani Simiyu kwa wanafunzi wa darasa la saba, kidato cha nne na
kidato cha Sita, ambayo ni madarasa yanayofanya Mitihani ya Taifa ya kuhitimu
elimu ya Msingi na Sekondari zitakuwa endelevu.
Mtaka amesema hayo Aprili 28, 2019 wakati akihitimisha Kambi ya
Kitaaluma kwa wanafunzi wa kidato cha sita iliyofanyika kwa takribani mwezi
mmoja katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, ikihusisha wanafunzi 1166
kutoka katika shule 12 mkoani hapa.
Amesema Mkoa utaendelea kufanya jitihada na kuboresha zaidi
kambi hizo huku akieleza kuwa ameshawaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote
mkoani humo kutenga fedha kwa ajili ya motisha kwa walimu na wanafunzi
watakaokuwa wakifanya vizuri.
“Kambi za kitaaluma zitaendelea kuwepo katika kipindi
chote nitakacho kuwepo na tutaendelea kuboresha; mwaka huu nimewaambia
Wakurugenzi ni lazima kila Halmashauri itenge fedha kwa ajili ya motisha katika
elimu, motisha kwa walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri” alisema Mtaka.
Katika
hatua nyingine Mtaka amewashukuru walimu, wanafunzi na wadau mbalimbali
waliochangia kufanikisha kambi ya kidato cha sita, huku akiwasisitiza wanafunzi
wa hao kuendeleza juhudi walizozionesha wakiwa kambini na kutumia
mbinu walizopewa na walimu mahiri ili waweze kufanya vizuri mitihani yao
ya mwisho.
Naye
Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato kutoka Jijini Mwanza, Nicodemo
Ntabindi amewaonya wanafunzi wa Kidato cha sita kutojihusisha na masuala ya
mapenzi badala yake wajikite katika masomo tu kwa sasa ili waweze kufikia ndoto
zao.
Kwa upande wao wanafunzi waliokuwepo katika kambi hiyo ya
Kitaaluma wamesema kambi hiyo imekuwa msaada kwa wanafunzi kwa kuwa imechangia
kuwasaidia kupata ufumbuzi wa mada ngumu zilizokuwa zinawapa shida na kuahidi
kufanya vizuri katika mtihani wa Taifa kutokana na namna walivyoandaliwa vema.
“Tunashukuru uwepo wa kambi hii maana imetusaidia kupata maarifa
ya namna ya kujibu maswali kwenye mitihani, lakini tumeweza kusaidiwa na walimu
kutatua mada ngumu ambazo zilikuwa zinatushinda, ninaamini kwa namna
tulivyoandaliwa hatutamuangusha Mkuu wetu wa Mkoa” alisema mwanafunzi Farida
Omary.
“Kambi hizi hazijafanyika popote hapa nchini tunamshukuru sana
Mkuu wa Mkoa kwa kuja na wazo la kuwa na kambi kwa sababu tumejifunza mengi,
tumekutana na wenzetu wa shule mbalimbali hapa mkoani kwetu na tukapata maarifa
ambayo awali hatukuwa nayo, tuna imani tufanya vizuri “ alisema mwanafunzi
Casto Nyakarungu.
Katika kambi hii Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu, imetoa shilingi
milioni 12 kwa ajili ya motisha kwa walimu waliokuwa wakifundisha kambini hapo
na imeahidi kutoa shilingi milioni nne kwa mwanafunzi atakayepata ‘division
one, pointi tatu’ na kuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora Kitaifa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment