METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, April 18, 2019

MHE HASUNGA ATOA WIKI MBILI KWA TUME YA MAENDEEO YA USHIRIKA KUFANYA UKAGUZI WA VYAMA VYA USHIRIKA WA KAKAO ILI KUDHIBITI UBADHILIFU

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha kujadili mustakabali wa zao la kakao na  zao la Kahawa, kilichofanyika katika ukumbi wa Kilimo IV Jijini Dodoma, Leo Tare 18 Aprili 2019. Wengine pichani ni Naibu Mawaziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa na Mhe Omary Mgumba(Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiongoza kikao kazi cha kujadili mustakabali wa zao la kakao na  zao la Kahawa, kilichofanyika katika ukumbi wa Kilimo IV Jijini Dodoma, Leo Tare 18 Aprili 2019.
Baadhi ya watumishi wa Wizara, Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakifatilia kikao kazi kilichoongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kujadili mustakabali wa zao la Kahawa.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Ndg Primus Kimaryo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa ubora wa kahawa na masoko Ndg Frank Nyalusi wakifuatilia kikao kazi kilichoongozwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kujadili mustakabali wa zao la Kahawa.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini imeagizwa ndani ya wiki mbili kufanya uchunguzi (Special auditing) wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Kakao ili kudhibiti ubadhilifu.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa agizo hilo leo tarehe 18 Aprili 2019 wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Kilimo IV Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Waheshimiwa Manaibu Waziri, Watumishi wa Wizara, Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Kyela, Kaimu Afisa Ushirika wa Wilaya ya Kyela na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kyela.

Mhe Hasunga amesema kuwa agizo hilo linapaswa kufanyiwa kazi kuanzia leo tarehe 18 Aprili 2019 na linapaswa kukamilika ifikapo tarehe 6 Mei, 2019 na punde zoezi hilo litakapokamilika taarifa ziwasilishwe kwake.

Baada ya kupokea maelezo ya wajumbe wote wakiwemo Naibu Mawaziri Mhe Innocent Bashungwa na Mhe Omary Mgumba na kujadiliana kwa kina mustakabali wa zao hilo pamoja na mambo mengine ametoa maelekezo mahsusi ili kuweza kuimarisha mfumo wa masoko ya zao la kakao.

Ameagiza kuanzia msimu ujao wa mwaka 2019/2020 wakulima wote wasajiliwe na kutambuliwa taarifa zao muhimu za kama ukubwa wa shamba analomiliki, pamoja na matarajio ya uzalishaji na wakulima kupatiwa kitambulisho.

Alisema katika msimu ujao pia kila Kijiji kimoja cha uzalishaji kiwe na AMCOS moja, hivyo Tume ya Maendeleo ya Ushirika iangalie Kanuni zilizopo ili kutekeleza suala hilo, ambapo agizo hilo linapaswa kuwa kwa AMCOS zote Tanzania sio zile za Kakao pekee.

Kadhalika, Mhe Hasunga ameagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau, ifanye uchambuzi wa kina na kupendekeza mfumo utakaotumika msimu ujao ambao utaonesha bayana makato halisi yaliyojumuishwa katika mjengeko wa bei.

Kadhalika, Waziri Hasunga amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Ndg Primus Kimaryo kujadili kwa kina Mfumo wa ununuzi wa kahawa unaotumika hivi sasa sambamba na upatikanaji wa pembejeo.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho pia kimejadili kwa kina namna ya kujipanga kwa ajili ya mfumo ujao wa msimu wa kahawa wa mwaka 2019/2020.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com