Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akichangia mada katika masuala ya kuboresha biashara huria barani Afrika wakati wa hitimisho la mkutano wa Africa Now Summit 2019 jijini Kampala, Uganda. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema huu ni wakati Viongozi
wa Afrika kuiangalia Afrika ijayo hivyo hakuna budi viongozi wa sasa kuandaa
mazingira ya Afrika bora na salama.
Makamu wa Rais ameyasema
hayo leo kabla ya kumalizia sehemu ya mwisho ya Mkutano wa Africa Now Summit 2019
unaofanyika kwenye hoteli ya Munyonyo Commonwealth Resort, Kampala nchini
Uganda.
Makamu wa Rais amesema
mkutano huo umeangalia suala zima la ongezeko la watu na uelewa wa vijana
katika maendeleo ya nchi zao haswa wakati huu wa uchumi wa viwanda ambapo pia
kuangalia mitaala ya elimu inayotolewa sasa kama inakidhi mahitaji ya kisayansi
na kiteknolojia.
“Lazima sasa
tuangalie hii idadi ya watu isije ikawa chanzo cha kuleta vurugu katika nchi
zetu bali iwe chanjo cha nguvu kazi kujenga nchi zetu”alisema Makamu
wa Rais.
Makamu wa Rais amesisitiza
kuwa Afrika ya sasa inahitaji Viongozi ambao hawajitazami wao bali wanatazama
wananchi wao katika makundi yao kama Vijana, Wanawake na Walemavu.
Makamu wa Rais pia
alikutana na kuzungumza na Naibu Rais wa Kenya Mhe. William Ruto ambapo baada
ya kikao hicho Makamu wa Rais amesema Tanzania na Kenya ni majirani pamoja na
kuwa kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wao kama nchi jirani lazima wahakikishe
uhusiano wao unasimama imara na kukuza ushirikiano.
0 comments:
Post a Comment