METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, March 11, 2019

AGHA KHAN BADILISHENI SKELI YA MISHAHARA-MAJALIWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Binti Mfalme Zahra Aga Khan  (wapili kushoto) wakifungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi, 9, 2019. Wengine kutoka kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zaynab Chaula, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na   kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa,  (Agence Francaise de Developpment), Christian Yoka. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es salaam, Machi 9, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Asema lengo ni kuondoa manung’uniko kwa watumishi wa taaluma moja

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Hospitali ya Aga Khan uandae skeli ya mishahara inayofanana kwa watumishi wenye taaluma zinazofafana ili kuondoa manung’uniko baina ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Ameyasema hayo kutokana na malalamiko ya watumishi wa taasisi hiyo ambao wanadai kuwepo kwa tofauti ya mishahara kwa watumishi licha ya kuwa na taaluma moja na kufanyakazi kwenye kituo kimoja.

Hayo yalisemwa jana (Jumamosi, Machi 9, 2019) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.

Waziri Mkuu alisema suala la maslahi kwa watumishi ni muhimu na linatiliwa mkazo na serikali hivyo uongozi wa Hospitali ya Aga Khan fanyeni mapitio ya mishahara hasa kwa watu walio katika taaluma zinazofanana.

“Serikali imeunda Tume ya Mishahara na Motisha inayofanya mapitio ya ngazi za mishahara ili kuondoa utofauti wa mishahara kwa watumishi waliosoma ngazi moja, wenye taaluma moja wanaofanyakazi kwenye kituo kimoja.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa suala la uwiano wa mishahara kwa watumishi wenye taaluma zinazofanana ni muhimu na linapaswa lifanywe kwa watumishi wote bila ya kujali kama mtumishi huyo ni Mtanzania au anatoka nje ya Tanzania. 

Awali, Waziri Mkuu alitembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma katika jengo hilo ikiwemo maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya wazazi. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu sh. bilioni 192, kati yake sh. bilioni 134 ni mkopo wa muda mrefu wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com