METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 19, 2019

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MWEKA HAZINA KIBONDO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo, Februari 19, 2019. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijadili jambo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati  alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo,  Februari 19, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya wilaya  ya Kibondo wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Februari 19, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Thomas Chogolo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma  zinazomkabili za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa halmashauri huyo kumaliza haraka migogoro yao ya kiutendaji kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kwani wanachokifanya ni kinyume na maelekezo yake.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo (Jumanne, Februari 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma.

“Katika Serikali hii suala la ukusanyaji wa mapato ni jambo nyeti na limepewa kipaumbele, hivyo ni lazima fedha inayokusanywa itumike kama ilivyokusudiwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.”

Waziri Mkuu amesema wananchi wa halmashauri hiyo wanalipa kodi kupitia kwa watendaji wa kata katika maeneo yao lakini  Mweka Hazina haingizi kwenye mfumo wa Serikali. “Jambo hili halivumiliki.”

Amesema mbali na fedha za makusanyo ya kodi pia matumizi ya fedha mbalimbali zinazopelekwa na Serikali katika halmashauri hiyo nayo hayaridhizishi. Ametoa mfano wa fedha za sekta ya Afya ambapo zaidi ya bilioni mbili zimepelekwa na dawa hakuna.

Waziri Mkuu amesema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma, hivyo amewataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imewapa dhamana watumishi hao kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si kutanguliza maslahi yao binafsi, amewataka wajirekebishe kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Serikali haitawapa nafasi ya kuendeleza migogoro yenu kila mmoja lazima atambue majukumu yake na kuyatekeleza. Serikali haiitaji mtumishi mvivu, masiyekuwa muadilifu na wala anayejihusisha na vitendo vya rushwa.”

Amesema ni lazima wakamaliza migogoro ya kiutendaji ambayo imesababisha watendaji wa halmashauri kutoelewana na kugawanyika katika makundi na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com