METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, January 15, 2019

Nyongo ataka wanaomiliki migodi kwa kuvamia wasimame mara moja


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiteta jambo na  Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Hashim Komba wakati akiondoka  katika eneo la mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata Wilaya ya Iringa, mara baada ya kuzungumza na wachimbaji wadogo na kutatua mgogoro uliokuwepo mgodini hapo.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akikagua mazingira ya shughuli za wachimbaji wadogo katika mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata wilayai Iringa. Naibu Waziri alifika mgodini hapo kwa ajili ya kutatua mgogoro baina ya mwekezaji na wachimbaji ikimweo pia kuzungumz na wachimbaji katika  mgodi huo.

Na Asteria Muhozya, Iringa


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wanaomiliki migodi kwa kuvamia maeneo bila kuwa na leseni, wasimame mara moja.

Naibu Waziri Nyongo ametoa kauli hiyo katika  mgodi wa Ulata kijiji cha Ulata wilayani Iringa , wakati wa ziara yake iliyolenga  kukagua shughuli za uchimbaji madini ikiwemo kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wadogo.

Aidha, kauli ya Naibu Waziri inafuatia mgogoro uliopo katika mgodi huo kati ya  mwenye leseni ya kumiliki mgodi huo Ibrahim Msigwa , wachimbaji wadogo wanaochimba katika eneo hilo na  Mansoor Almasi anayetajwa kuwa mmiliki mwingine na mnunuzi wa madini  ya dhahabu yanayochimbwa mgodini hapo ambaye kwa mujibu wa taratibu,  hana  vibali  vinavyomruhusu kufanya shughuli hizo.

Akilenga kutatua na kuumaliza mgogoro uliopo mgodini hapo, Naibu Waziri amemtaka Mansoor Almas, kufika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa ifikapo Januari 15, na endapo atakiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“ Sisi kama serikali ambao ndiyo tunatoa vibali tunamtambua bwana Msigwa kuwa ndiye mmiliki halali. Nataka kuonana na huyu Mansour na yoyote anayedharau serikali tutakula nae sahani moja,” alisisitiza Naibu Waziri. 

Naibu Waziri alisema lengo la kutaka Mansour kufika wilayani hapo ni kutaka kusikia kutoka pande zote ili  mgogoro huo uweze kutatuliwa na kufika mwisho jambo ambalo litawezesha  shughuli za uchimbaji katika eneo husika kuendelea vizuri  ili pande zote yaani serikali na wachimbaji wanufaike.

Akifafanua kuhusu suala la shughuli za uchimbaji, Naibu Waziri amesisitiza kuwa, ili kuwa mchimbaji halali ni lazima kuwa na kibali kutoka serikalini na kuongeza kwamba, ni vigumu kuomba kwenye leseni ya mtu mwingine.

Pia, amewataka wachimbaji wadogo kutoshirikiana na wale wote wanaopindisha  utekelezaji wa sheria na taratibu katika shughuli za uchimbaji madini na badala yake washirikiane na wale wenye vibali vya umiliki  kutoka serikalini.

Pia, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wale wote wasiokuwa na uwezo wa kuchimba kuingia mikataba na wachimbaji wengine wenye uwezo ili kuwezesha lengo la kumiliki leseni kutimia kwa kuhakikisha kwamba zinafanyiwa kazi. “ unaweza kuingia mkataba na mchimbaji  wengine wakiwemo wa kati.

“ Nataka muelewe kwamba, mnaochimba mnachimba kwa niaba ya watanzania kwa sababu watanzania ambao siyo wachimbaji. Hawa wanafaidika kutokana na kodi na mrabaha unaolipwa kutokana na shughuli zenu, kwa kuwa fedha hizo zinatumika katika kutoa huduma nyingine,” alisema Nyongo.

Awali, wachimbaji hao waliwasilisha kero kwa Naibu Waziri kuhusu mgogoro wa umiliki wa mgodi huo umesababisha shughuli za uchimbaji mgodini hapo kuwa mgumu suala ambalo linasababisha ugumu wa kupata kipato cha kujikimu na kuendesha familia zao.

Wachimbaji wao walimshukuru Naibu Waziri kwa kufika kwake mgodini hapo  ambapo walipata fursa ya kueleza kero ikiwemo  suala la bei elekezi ya madini hayo ambalo walimlalamikia kuwa, wamekuwa wakiwauzia wanunuzi wa  madini hayo akiwemo Mansoor Almasi na Ibrahim Msigwa kwa kiasi cha shilingi 45,000 kwa gramu moja jambo ambalo Naibu Waziri ameeleza kuwa, atakapoonana na wahusika hao atawaeleza kuhusu suala hilo.

Akitoa utetezi wake kwa Naibu Waziri kuhusu kero zilizowasilishwa dhidi yake na wachimbaji hao, Msigwa amesema mazingira mabaya mgodini hapo yaliyowasilishwa na wachimbaji yanatokana na kuwepo kwa kesi mahakamani jambo ambalo linamfanya ashindwe kuendelea na shughuli za uchimbaji kama inavyompasa.

 Wakati huo, huo,  katika kikao na uongozi wa Mkoa wa Iringa, Katibu Tawala wa Mkoa huo Happines Seneda, alimweleza Naibu Waziri kuhusu umuhimu wa kuwa na Afisa Madini wa Mkoa huo badala ya kutegemea AFisa Madini wa Mkoa wa Njombe jambo ambalo ameeleza kwamba, uwepo wake mkoani humo utaongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa shughuli za madini.

Akijibu ombi hilo, Naibu Waziri Stanslaus Nyongo alimweleza  Katibu Tawala huyo kuwa, Wizara imelenga kuhakikisha kwamba kila Mkoa unakuwa na Afisa Madini baada ya kuondolewa kwa Makamishna wa Madini wa Kanda kufuatia Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Maboresho yake ya Mwaka 2017.


Naibu Waziri Nyongo alitembelea mgodi huo Januari 14, 2019.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com