Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.
Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la
wadau wa asasi za maendeleo ya vijana nchini walipokutana kujadili maendeleo ya
vijana kupitia programu ya
mabadilishano ya vijana (Exchange Program) kati ya Nchi ya Ujerumani na
Tanzania. Kongamano hili limefanyika hoteli ya Morena Januari 16, 2019,
Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe.
Jenista Mhagama akipata maelezo kuhusu taulo za kike kutoka kwa Bi. Josephine
Lyengi, alipokuwa akiangalia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na vijana.
(Kulia) ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
Bi. Beng’i Issa, (Kushoto) ni Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC) Bw.
Lenin Kazoba.
Na; OWM (KVAU), Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista
Mhagama amezitaka asasi mbalimbali zinazoshughulikia maendeleo ya vijana kuwa
chachu ya maendeleo nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la
wadau wa asasi za maendeleo ya vijana nchini walipokutana kwa lengo la kukuza
uelewa katika kutekeleza programu ya kuwawezesha vijana kati ya Ujerumani na
nchi za Afrika (African – German Youth Initiative), Waziri Mhagama alisema
kuwa, Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana na Sera ya Taifa ya
Ajira imekuwa ikihamasisha wadau mbalimbali kuanzisha Miradi na Programu
zinazowawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu wa kuwaweza kujiajiri au
kuajiriwa katika Sekta mbalimbali ili waweze kuchangia kwenye maendeleo ya nchi.
“Vijana ndio chachu kubwa ya maendeleo endelevu,
hivyo ni vyema wakatumia fursa zilizopo kuleta mabadiliko yatakayo kuwa na tija
na mchango kubwa katika maendeleo ya taifa.” alisisitiza Mhagama
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa vijana
wanawezeshwa ipasavyo kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Pia alifafanua kuwa, Serikali imekuwa ikishirikiana
na wadau wanaoshughulika masuala ya maendeleo ya vijana katika kuwajengea ujuzi
na uelewa vijana juu ya maendeleo. Hivyo aliipongeza Taasisi ya vijana ya
Tanzania Youth Coalition katika kujenga ustawi na maendeleo endelevu kwa vijana
ambao ndio wanufaika wa fursa ya programu hiyo ya mabadilishano ya vijana na
Mataifa mengine.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa vijana nchini
kufanya kazi kwa bidii na kuendelee kudumisha uzalendo, amani na utulivu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa
la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa alieleza kuwa Programu
ya mabadilishano ya vijana (Exchange
Program) imekuwa na manufaa makubwa sana katika kuwajengea uwezo
vijana kupitia fani mbalimbali zinazoleta mabadiliko ya chanya katika Taifa.
Naye, Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC)
Bw. Lenin Kazoba alisema kuwa kongamano hilo litakuwa na manufaa kwa vijana na
asasi zinazoshughulikia maendeleo ya vijana kwa kuweza kujadili kwa pamoja
fursa zitakazoleta maendeleo kwa vijana na jamii inayowazunguka.
Programu ya mabadilishano ya vijana kati ya
Nchi ya Ujerumani na Tanzania ilizinduliwa rasmi tarehe 30 Juni, 2016
Mjini Bonn, Ujerumani na Waziri wa Uchumi wa Ushirikiano na Maendeleo Mhe. Gurd
Muller ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu ilikuwa moja kati ya Nchi Tatu (3) Barani Afrika zilizopewa heshima
kubwa ya kuchaguliwa kutekeleza mradi huo kwenye hatua ya majaribio kupitia
Tanzania Youth Coalition (TYC). Zaidi ya vijana 4,015 wamefaidika kupitia
program hiyo kwa kupata ujuzi na uzoefu wa fani mbalimbali.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment