METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, October 19, 2018

DK.KALEMANI AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MAFUTA WA DRC

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa Aime Ngoi-Mukena (kushoto) akitembelea miundombinu ya bomba la Tazama ili kupata ufahamu kuhusu uendeshaji wa Bomba hilo refu.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akiwa na Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa  Aime Ngoi-Mukena (kulia) na Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini DRC,  Michael Sereki.
               .............................................................
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 18 Oktoba, 2018, amekutana na Waziri waMafuta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Profesa  Aime Ngoi-Mukena ambapo wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa siku za nyuma ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Waziri wa Nishati, jijini Dar es Salaam yalijikita katika kujadili sehemu kuu nne za ushirikiano ambazo ni kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa Tanganyika, usafirishaji mafuta safi kutoka bandari ya Tanga na Dar Es Salaam na utumiaji wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) kwa ajili ya mafuta kutoka DRC katika Ziwa Albert.

Eneo jingine walilojadili ni ushirikiano wa wataalam wa Sekta ya Mafuta na Gesi wa nchi hizi mbili ili kuongeza uelewa na kupata uzoefu wa kazi.

Waziri wa Nishati wa DRC, alitumia fursa hiyo kuomba msaada wa watalaam wa gesi wa Tanzania  kwenda kufundisha vijana nchini DRC baada ya nchi hiyo kufungua Chuo Kikuu cha Mafuta na Gesi.

Kwa upande wake, Dkt Kalemani alimweleza Waziri huyo wa DRC kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kujali ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na DRC na hivyo Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande  mbili yanatakelezwa na kuleta manufaa kwa Wananchi wa Tanzania na DRC.

Kwa pamoja Mawaziri hao waliwaelekeza watalaam wa Wizara ya Nishati kutoka Tanzania na DRC pamoja na  Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa pamoja waandae  mpango kazi wa kutekeleza makubaliano hayo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Watalaam wa Wizara ya Nishati ya Tanzania na DRC, Mwakilishi kutoka Ubalozi wa  Tanzania nchini DRC na TPDC.

Waziri wa Nishati wa DRC, pia alipata fursa ya kutembelea miundombinu ya kupakulia mafuta katika Gati ya Kurasini, SPM na baadaye kutembelea miundombinu ya bomba la Tazama ili kupata ufahamu kuhusu uendeshaji wa Bomba hilo refu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com