Muuguzi Neema Mlay akitoa chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa mwanafunzi Happiness Robert wa Shule ya Sekondari Simiyu wakati wa Uzinduzi wa chanjo hiyo Mkoa wa Simiyu katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B Mjini Bariadi, (kulia) Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka akishuhudia zoezi hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Mjini Bariadi wakati wa uzinduzi wa Utoaji wa chanjo ya Saratani ya mlango wa Kizazi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B Mjini Bariadi.
Flora Masunga mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sima B akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) baada ya kupata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi mara baada ya uzinduzi wa Utoaji wa chanjo hiyo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B Mjini Bariadi.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Simiyu, Baetrice Kapufi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya Uzinduzi wa zoezi la chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Sima A na Sima B Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga,
Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony
Mtaka amezindua rasmi leo zoezi la chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi
ambayo inatarajiwa kutolewa kwa watoto wa kike takribani 37,141 wenye umri wa
miaka 14 kwa mkoa mzima wa Simiyu.
Uzinduzi huo umefanyika katika Uwanja wa
Shule ya Msingi Sima A na Sima B na kushirikisha watoto wenye umri wa miaka 14
kutoka katika baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari za Halmashauri ya Mji wa
Bariadi.
Akizungumza
na wanafunzi walioshiriki katika uzinduzi wa chanjo hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa
amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wa kuwahamasisha wenzao kwenda kupata
chanjo na kuwahamasisha wazazi kuwahimiza watoto wa kike wote wenye umri wa
miaka 14 kwenda kupata chanjo hiyo.
Mratibu
wa Chanjo Mkoa wa Simiyu Bibi.Beatrice Kapufi ametoa wito kwa wazazi na walezi
kuhakikisha watoto wenye umri wa miaka 14, wanapata haki yao ya kupata chanjo ya Saratani
ya Mlango wa Kizazi ambayo itatolewa bila malipo katika vituo vya kutolea
huduma za afya, shule za Msingi na Sekondari.
Aidha,
amesema Mkoa kupitia Kitengo cha Huduma za Chanjo wameshatoa mafunzo kwa
watendaji, watoa huduma wote wa vituo vinavyotoa huduma ya chanjo na walimu wanaojishughulisha
na huduma za Afya katika Shule za Msingi na Sekondari zote mkoani Simiyu.
“Nitoe
wito kwa wazazi wote kuhakikisha watoto wa kike wote wenye miaka 14 wanapata
haki yao msingi kupata chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi, chanjo hii inatolewa
bure na itatolewa mara mbili, mtoto akishapata kwa mara ya kwanza atatakiwa
kwenda kupata chanjo ya pili baada ya miezi sita” alisema Kapufi.
Nao
wanafunzi waliopata chanjo wameishukuru Serikali kwa kuwaletea chanjo hiyo
ambayo wamesema itawasaidia kujikinga na maambukizi ya Saratani ya Mlango wa
Kizazi.
“Tunashukuru
sana Serikali kwa kutuletea chanjo hii itatusaidia tusipate Saratani ya Mlango
wa Kizazi, nawaomba wazazi wawaambie wenzetu nao waende wakapate chanjo hiyo, ili wasipate Saratani wakiwa wakubwa” alisema Flora
Masunga mwanafunzi wa Shule ya Msingi Sima B.
0 comments:
Post a Comment