METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 7, 2018

"MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI; WANAWAKE WATUMIE VIPAJI NA UTAALAMU KUNYANYUA UCHUMI WA TAIFA"

Na Debora Charles✍๐Ÿฝ

Ibara ya 124(1) (b) ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 1977 Toleo la 2017 inatambua umuhimu wa kuwepo kwa Jumuiya ya Wanawake ambayo ni “Umoja wa Wanawake Tanzania”- UWT. Ni wazi kuwa uwezo wanawake kutambulika na kupewa chombo pekee cha kujiongoza kwenye Chama kinachotoa uongozi wa nchi ni ishara inayodhihirisha wazi kuwa MWANAMKE ni NGUVU na NGUZO YA MAENDELEO katika jamii. Aidha Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwezi Agosti mwaka 2012, ilionyesha kuwa Idadi ya Wanawake Tanzania Bara ni 23,058,933 na wanaume ni 21,869,990. Wingi wa idadi ya kundi hili ni picha halisi kuwa wanawake ni FURSA na MITAJI ya kuliletea Taifa MAENDELEO endapo watatumika ipasavyo.

Siku ya Maadhimisho ya Wanawake Duniani kupitia Umoja wa Mataifa (UN), ilianza rasmi mwaka 1975 ambapo miaka miwili baadaye, Desemba mwaka 1977, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha na kutangaza kuadhimisha Siku hiyo kama ni siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa. Sherehe hii humtambua kila mwanamke kwa mafanikio yake bila kuegemea upande wowote kitaifa, kikabila, kiuchumi, kilugha au msimamo wake wa kisiasa. Kwa sasa zaidi ya nchi 100 zinaadhimisha siku ya wanawake duniani na baadhi ya nchi wameitangaza kama siku rasmi ya mapumziko.

Katika nchi yetu ya Tanzania siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1996 ambapo kila mwaka hufanyika katika ngazi za Mikoa na kitaifa kila baada ya miaka 5. Mwaka huu, siku hii inaadhimishwa kwa ngazi za mikoa na Kaulimbiu ya Taifa ni "Kuelekea uchumi wa viwanda tuimarishe usawa wa kijinsia na uwazeshaji na wanawake vijijini" Bado kuna uhitaji wa kufikisha elimu ya kijinsia kwa wingi vijijini ili wanawake waweze kuondokana na ukatili na unyanyasaji kutoka kwa wanaume na hasa waume zao.

Ni dhahiri kuwa maadhimisho haya yamekuwa yakichochea kwa kiasi kikubwa kiwango cha MAFANIKIO ya mwanamke nchini na Duniani kote. Wanawake sasa wanashiriki katika vyombo vya juu vya maamuzi. Tanzania sasa inajivunia kuwa na Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke (MAMA SAMIA SULUHU HASSAN) kuwahi kutokea nchini ambaye aliupata wadhifa huo kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliomuweka Rais Dkt. John Pombe Magufuli madarakani.

Kadharika mafanikio ya usawa wakijinsia yameongezeka katika mitazamo ya Elimu, umiliki wa Ardhi na hata Uchumi kuanzia ngazi za familia. Kwa kiasi kikubwa mwanamke wa sasa anapata HAKI YA ELIMU, ana SAUTI YA MAAMUZI na ana uwezo wa KUMILIKI UCHUMI.

Hata hivyo, siku hii inaendelea kung’ara kutokana na wanawake wengi kujitokeza kuwania fursa za kimaendeleo katika Nyanja mbalimbali za maisha. Wapo wanawake wengi mashuhuri Afrika wanaofanikiwa kutokana na juhudi walizonazo na kuwa hamasa ya mafanikio kwa wengine. Katika Orodha ya Forbes ya wanawake 100 mashuhuri zaidi na wenye ushawishi zaidi duniani mwaka 2016, kuna wanawake watatu kutoka Afrika waliibuka miongoni mwao. Wanawake hao walikuwa ni;

FOLORUNSHO ALAKIJA, mwanamke ambaye Utajiri wake ulikuwa ni Bilioni 1.73 ya Dola za Kimarekani na ni mwanamke wa pili kwa utajiri Afrika baada ya Isabela Dos Santo ambaye Mwaka 2013, kutokana na utafiti uliofanywa na Forbes, utajiri wake ulikuwa ni zaidi ya Bilioni 3 ya Dola za Kimarekani. Folorunsho alianza katika MITINDO na baadae akajizolea utajiri katika mafuta.

ELLEN JOHNSON SIRLEAF, mwanamke aliyekuwa Rais wa Liberia tangu 2006 na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel. Aliwahi kuwa Kiongozi wakati wa mlipuko mbaya zaidi wa Ebola duniani pamoja na AMEENAH GURIB FAKIM yeye ni Mwanamke wa kwanza kuwa Rais Mauritius, wadhifa ambao sana ni wa staha na ni mwanasayansi anayetambulika duniani akiangazia sana uhifadhi.

Ni dhahiri kuwa wanawake wakionyeshwa fursa na kupewa uhuru wa kuzitumia huleta ushawishi mkubwa kwenye jamii hususani kwa wanawake wenzao wanaowazunguka. Professor Ester Mwaikambo, Mwanamke wa kwanza Tanzania kuwa Daktari Bingwa (alipata shahada ya udaktari mwaka 1969 nchini Urusi) aliyebobea kwenye magonjwa ya watoto huku pia akiwa mmoja wa waanzilishi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), ameweza kufanikisha malengo yake kwa kiwango kikubwa katika sekta ya Afya na Elimu kwa mtoto wa kike hasa kuhusu somo la Sayansi.

Tunapoadhimisha siku hii, Ni lazima wanawake tukumbuke kuwa na NGUVU YA PAMOJA (Joint Power) itakayotusaidia kupanua wigo wa fikra na ushirikiano, tufanye vitu kwa UTAALAMU hususani katika biashara zetu, tutambue kuwa ELIMU NI VIPAJI ni jukumu letu kutambua na kukuza vipaji vyetu, tutambue mahitaji yetu HALISI ili itusaidie kitatua haja zetu kwa usahihi, tuondokane na dhana ya utegemezi hususani kwenye ngazi za familia ili tuendane na mahitaji ya dunia ya sasa.

Ni lazima wanawake tuwekeze kwenye KILIMO. Tuwe na mikakati mizuri kwenye USHINDANI WA MASOKO, tuongeze thamani ya mazao yanayolimwa na tufanye kilimo kiwe KITAMU NA KIPENDWE na jamii kupitia mavuno yanayozalishwa. Tafiti zinaonesha kuwa Mabilionea wengi wa vizazi vijavyo Afrika watakuwa ni WAKULIMA. Hii inatupa tafsiri ya wazi kabisa kuwa kilimo ni UTAJIRI, kilimo ni FURSA na kilimo KIINI CHA MAENDELEO.

Tuwe na MUENDELEZO wa shughuli tunazozianzisha, tusiruhusu mitazamo ya watu wengi kuwa vikwazo kwenye kazi zetu, Tuwe watafutaji wa MAARIFA NA TAARIFA kwa wakati na kwa usahihi. Tutumie fursa zinazotolewa na Serikali (hususani fungu la wanawake kwenye mapato ya Halmashauri za wilaya), KUJIIMARISHA. Tujitoe, tukubali kujifunza, tuwe na ndoto, tushughulike na nafasi tulizonazo na kuonyesha uwezo wetu popote tulipo, tuwe tayari kuthubutu, tuwe JASIRI NA TUJIAMINI hususani katika kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
Tuthamini dhamana tunazopewa huku tukijua kuwa ni fursa zetu za kuweza kutekeleza MAENDELEO.

Tuhamasishane sisi kwa sisi kwenye kushiriki shughuli za maendeleo na kushiriki KUGOMBEA nafasi mbalimbali za Uongozi. TUSIKWAMISHANE, tupongezane na kukosoana kwa malengo mema ya kujenga na kamwe tusishiriki KUKANDAMIZA haki zetu hususani katika masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo UKEKETAJI.

Tarehe 08/03/2018 iwe FURSA kwa wadau wote wa wanawake kuwekeza kwenye elimu ya STADI ZA MAISHA hasa kwa MSICHANA ili kujenga dhana ya kuthamini vipaji kwa vizazi vijavyo. Aidha iwe fursa kwa wadau wote wa ELIMU YA KIJINSIA kuelimisha wanandoa vijijini kuhusu madhara ya UNYANYASAJI wa kijinsia.

HERI YA SIKU YA WANAWAKE DUNIA, HERI YA SIKU YA WANAWAKE TANZANIA

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com