Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Tixon Nzunda akifungua mafunzo kwa walimu wa
shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu , Maofisa wa
Ustawi wa Jamii na Maofisa Elimu Maalum ngazi za wilaya na Mikoa
yote ya Tanzania Bara mjini Morogoro jana.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo ambao ni walimu wa shule
zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu , Maofisa wa
Ustawi wa Jamii na Maofisa Elimu Maalum ngazi za wilaya na Mikoa
yote ya Tanzania Bara wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa
mafunzo mjini Morogoro jana.
Paulina Mkwama, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI,
akitoa maelezo ya awali wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa
walimu wa shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu ,
Maofisa wa Ustawi wa Jamii na Maofisa Elimu Maalum ngazi za wilaya
na Mikoa yote ya Tanzania Bara mjini Morogoro jana.
Na Fred J. Kibano
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu,
Tixon Nzunda amefungua mafunzo kwa walimu wa shule
zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu,Maofisa wa Ustawi wa Jamii
na Maofisa Elimu Maalum ngazi za wilaya na Mikoa yote ya Tanzania
Bara.
Akifungua mafunzo hayo ya siku sita mjini Morogoro, Nzunda
amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI imepanga kufanya zoezi maalumu
la kuwatambua watoto wenye ulemavu wa aina tofauti ili
watabuliwe kwa ajili ya kupata afua sahihi na mahitaji
maalumu ya kielimu mashuleni.
Amesema mafunzo hayo
maalum yamelenga kuwapatia mbinu mbalimbali za kuwatambua na
kuwafichua watoto wenye mahitaji maalumu ili nao wapatiwe fursa ya elimu kama
watoto wengine.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kutoa
Elimu Bila Malipo na bila vikwanzo
vyovyote, lakini pia kwa kutumia fursa hiyo, Serikali kwa kupitia
Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendesha zoezi la muda wa siku 21 katika
mikoa yote ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuwatambua
watoto wenye mahitaji maalumu kulingana na ulemavu walio nao ili wapate elimu.
Nzunda alisema kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja zimetengwa
kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa watoto hao na
kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa waadilifu mkubwa
,wawajibikaji , wasikivu kwa walezi na wazazi wa watoto hao , na
walimu wa shule husika ili kupata takiwmu sahihi ya aina ya
ulemavu na mahitaji yao.
Paulina Mkwama, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu Ofisi ya Rais
TAMISEMI, alisema Serikali chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI
imekusudia kuendesha zoezi la kuwatambua watoto wenye mahitaji maalumu ili
kupata afua sahihi na mahitaji ya kielimu na uhitaji
unaoongezeka kwa kundi hilo nchini.
Mkwama alisema, tangu mwaka 1998 Serikali iliporidhia matamko ya
kimataifa ya Elimu Jumuishi (Inclusive Education) hakukuwepo utaratibu maalum
wa kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu na hivyo kupelekea kundi hilo la
watoto kutopata elimu inayostahili kwa kuzingatia afua sahihi ya aina ya
ulemavu walionao.
Mkwama alisema , miongoni mwa watoto wenye mahitaji
maalumu ambao wanatakiwa kutambuliwa ni wenye
ulemavu wa viungo, walemavu wa ngozi, wenye mtindo wa ubongo,
wasioona, uoni hafifu , viziwi , wasioweza kuongea na wenye usonji.
Aidha, Mkwama alisema, kuwepo kwa vitendo vya wazazi kuwaficha
watoto wenye matatizo ya akili na usonji ni miongoni mwa sababu ya
watoto hao kukosa haki ya msingi ya kupata elimu bora na kuwapelekea
kuishi kwenye mazingira magumu.
Utambuzi huo utafanyika katika ngazi ya shule na kwenye jamii
ili kuwaibua watoto wenye mahitaji maalumu kuanzia miaka minne na zaidi
waliofichwa ili waibuliwe na kuweza kupatiwa elimu inayohitahiki kwao.
Pia takwimu zitakazoandaliwa zitawasilishwa katika mamlaka za
juu ili zifanyiwe kazi ya uchambuzi wa mahitaji halisi.
0 comments:
Post a Comment