METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, January 14, 2018

WANANCHI WATAKIWA KULIPA KIPAUMBELE ZOEZI LA URASIMISHAJI MAKAZI

Wananchi wametakiwa kulipa kipaumbele zoezi la urasimishaji wa makazi  ili kuongeza thamani ya  ardhi yao na kuepeka kero zinazoweza kujitokeza mara baada ya kuzinduliwa kwa mpango kabambe wa mji wa Mwanza

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula alipokuwa akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu wa kata ya Ilemela na Kawekamo akieleza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuchaguliwa kwake ambapo amewataka wananchi kulipa kipaumbele zoezi la urasimishaji makazi na kuhakikisha wanalipia hati miliki kabla ya uzinduzi wa mpango kabambe wa mji wa Mwanza kuepuka kuvunjiwa nyumba zao na kero nyengine zinazoweza kujitokeza kwa kwenda kinyume na matumizi ya ardhi ya mpango kabambe huo

‘… Nawaambieni ndugu zangu ili mpate nguvu ya zoezi hili la urasimishaji mnatakiwa mlipie na hati,  Msiridhike kwa kuwekewa tu vigingi baada ya kupimiwa hakikisheni mnapata hati hili jambo ni lazima mlipe kipaumbele msipofanya hivyo tutakuja kulaumiana bila sababu huko mbele ardhi ni mali,  ardhi ni mtaji hakikisheni mnapata hati …’  Alisema

Aidha Dkt Angeline Mabula amezitaja faida za kuwa na hati miliki ya ardhi kwa wajumbe hao kuwa ni pamoja na kulipwa fidia inapotokea kuna matumizi tofauti ya ardhi husika  na matakwa ya mpango kabambe na  kuwa kama mtaji katika shughuli za uwekezaji, kutumika kama dhamana kwa maendeleo binafsi  huku akikemea vitendo vya baadhi ya wenyeviti wa mitaa kutokuwa waaminifu kwa kupima na kuuza maeneo ya umma yaliyokuwa wazi kupitia zoezi hilo la urasimishaji makazi ambapo ameagiza kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua mwenyekiti wa mtaa Nyasaka A kwa kitendo chake cha kutapeli mwananchi kwa kumuuzia eneo lisilokuwa lake

Nae diwani wa kata ya Kawekamo Mhe Japhes Rwehumbiza amemshukuru mbunge huyo kwa ziara hiyo ya utekelezaji wa Ilani na ushirikiano anaoupata huku akitaja miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa katika kata yake kwa msaada wa Mhe mbunge

Katika ziara hiyo Mhe Dkt Angeline Mabula ameongozana na viongozi wa CCM wilaya ya Ilemela na jumuiya zake wakiongozwa na katibu wa Itikadi na Uenezi Dennis Kankono, diwani wa kata husika na wataalamu wake  huku zoezi la urasimishaji makazi likitegemewa kufika tamati mapema mwezi Juni 30, 2018

‘Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
15.01.2018

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com