Judith Ferdinand, Mwanza
Uongozi wa timu ya Alliance FC ya jijini Mwanza inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (FDL), imempogeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Harrison Mwakyembe kuingilia kati na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua kuhusiana na kilichotokea katika mechi mbili za ligi hiyo zilizochezwa desemba 30 2017.
Katika mechi hizo zilizochezwa katika viwanja tofauti zilitawaliwa na figisufigisu na kupelekea mashabiki na wapenzi wa soka kulalamika ambapo Dodoma FC ilikutana na Alliance FC (Mwanza) iliyochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma na Pamba FC (Mwanza) na Biashara (Mara) iliyochezwa Musoma na katika michezo hiyo ilionekana kuwa na maamuzi yasiyo ya haki na yenye upendeleo kwa timu ambazo ni wenyeji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Mashindano wa timu ya Alliance Yusuph Budodi alisema hatua zilizochukuliwa na Dk.Mwakyembe ni jema na anaimani TFF pamoja na Rais wake Wallace Karia itafanyia kazi agizo hilo na haki itapatikana.
“Nampongeza Dk.Mwakyembe kwa hatua alizochukua kwa kuiagiza TFF kuchukua hatua dhidi ya malalamiko yaliyojitokeza katika mechi mbili zilizopingwa mwishoni mwa mwaka jana, kwani ni jambo jema kwa maslahi ya soka nchini,hivyo aliiomba naimani na shirikisho hilo pamoja na Rais wake Wallace Karia kuwa watalifanyia kazi agizo hilo na haki itapatikana,” alisema Budodi.
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa timu ya Alliance Kessy Mziray (pichani) alisema mchezo huo dhidi ya Dodoma FC ambao waliibuka na ushindi wa goli 3-2 ulijaa upendeleo wa wazi na kutofuatwa sheria 17 za soka ambapo alidai walifanyiwa hujuma kwa mechi hiyo kuchezeshwa dakika 104, huku wachezaji watatu wakitolewa nje kwa kadi nyekundu na mmoja akipewa kadi nyekundu akiwa nje ya uwanja.
“Tumekata rufaa kupinga vitendo ambavyo siyo vya kiungwana dhidi ya mchezo wetu na Dodoma FC pamoja na kadi nyekundu zilizotolewa kwa wachezaji wetu wanne ni hujuma na kwa nini? walikataa mchezo huo usirekodiwe na waandishi wa habari, na ukitazama matukio yote yaliyofanyika katika mechi hiyo utaona kuna ‘figisufigisu’ nyingi zilizofanywa dhidi yetu,” alisema Mziray.
alisema, vijana wao wamejengwa kiufundi na kiakili na wana maadili ya hali ya juu kwani haijawahi kutokea wachezaji zaidi ya wawili kupewa kadi nyekundu kwenye mchezo mmoja, hivyo wanadhani baada ya viongozi kuona uwezo wa wenyeji ni mdogo wakaanzisha hujuma za kuwapunguza wageni uwanjani.
“Tangu tumeanza ligi siyo mwaka huu tu haijawahi kutokea vijana zaidi ya wawili, katika timu yetu kupewa kadi nyekundu kwani tumewajenga kiakili, kiufundi na maadili ya hali ya juu, inasikitisha,inakatisha tamaa na inaumiza kwani tunafanya kazi katika jua na mvua ili kuandaa vijana ila mtu anakuja ndani ya dakika 90 anakunyang’anya haki yako,” alisema Mziray.
0 comments:
Post a Comment